Walimu wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela wametakiwa kuhakikisha wanasimamia nidhamu na maadili ya wanafunzi sambamba na kuzidisha bidii katika ufundishaji.
Kauli hiyo imetolewa na Mhe Hassan Masala Mkuu wa Wilaya ya Ilemela katika kikao kilichowakutanisha wadau wa elimu kwa lengo la kutathmini hali ya elimu wilayani Ilemela.
“Tusimamie nidhamu ya watoto wetu, ni wajibu wetu tutimize hilo, tujitahidi kulinda usalama wa watoto wetu kesi za ulawiti zimekuwa nyingi sana hivyo watoto wetu hawapo salama sana, tunalo jukumu la kuweka mkakati wa pamoja wa kuwalinda watoto ikiwa ni pamoja na kuzikagua shule zetu” amesisitiza Mhe Masala
Mhe Masala ameendelea kusisitiza kwa kuwataka walimu kuongeza bidii katika ufundishaji, kwani ni matamanio yake kuona Ilemela inashika nafasi ya kwanza kimkoa, amesisitiza
Aidha ili kuweza kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi katika shule, Mhe Masala amewataka waheshimiwa madiwani kuwahamasisha wananchi juu ya ujenzi wa madarasa mapya.
“Kuna madarasa lazima tuyaongeze nikuombe Mstahiki Meya kwenye vikao vyenu muweke mkakati wa kuona namna ambavyo tutajenga madarasa mapya kwani tunao upungufu wa vyumba vya madarasa 193. Ni matarajio na matamanio yetu kuona tunazimaliza hizi changamoto, na yote yanawezekana kama dhamira yetu tunaiweka inakuwa ni kitu kimoja”, Amesema Mhe Masala
Akichangia katika kikao hicho Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii na diwani wa kata ya Ibungilo Mhe Hussein Magera ameomba nguvu zaidi ielekezwe sekta ya elimu msingi kwani bado changamoto ni kubwa ya upungufu wa madarasa na madawati huku akishauri juu ya kubadili mfumo wa ujenzi wa madarasa kutoka madarasa ya kusambaa na kujenga mfumo wa ghorofa ili kuweza kuhifadhi maeneo katika shule zetu.
Ummy Wayayu ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela nae amewahimiza walimu kuhakikisha watoto wanafundishwa stadi za maisha kuanzia wakiwa na umri mdogo ili watakapokuwa watu wazima wakayaishi mafundisho hayo
“Unapomfundisha mtoto akiwa mdogo ataenda kuyaishi maisha hayo akiwa mkubwa hivyo walimu tunaokaa na hawa watoto tuangalie namna ya kuwakuza katika njia bora”
Bi Sitta Kirawe ni Mkuu wa shule ya sekondari Nundu na Bwana Nashir Wamuraza mwalimu mkuu shule ya msingi Buzuruga D wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kikao chenye tija katika kuboresha elimu Ilemela na kuahidi kwenda kutekeleza yale waliyoelekezwa kwa kushirikiana na wadau wengine kwenye kata wakitolea mfano juu ya ya namna watakavyodhibiti suala la utoro wa walimu na watoto kwa kushirikisha wazazi na kamati za shule ikiwa na pamoja na kushirikisha uongozi wa kata
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.