"Nimefanya kazi hapa miaka 4 kwa mara ya kwanza niliteuliwa tarehe 21 Juni 2021 na kwa muda niliokaa hapa ninayo mengi ya kusimulia, mengi ya kuyasema na mengi ya kushuhudia, itoshe kuwashukuru wote tuliofanya kazi kama timu moja kwa ajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo la wilaya ya Ilemela na mkoa wa mwanza kwa ujumla"
Ni kauli ya Mhe Hassan Elias Masala aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela wakati akimkabidhi ofisi rasmi Mkuu mpya wa Wilaya ya Ilemela Mhe Amir Mohamed Mkalipa, siku ya Jumatatu tarehe 14 Julai 2025, huku akiwataka watumishi kuendeleza ushirikiano waliokuwa wakimpatia wakati wa uongozi wake akiwa wilayani hapa.
Sambamba na hilo ameishukuru Kamati ya Usalama ya Wilaya, Kamati ya siasa ya Wilaya, Mbunge wa jimbo na Mkurugenzi na timu yake ya watumishi kwa ushirikiano wao waliompatia katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Nae Mhe Amir Mkalipa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela akiongea na hadhira iliyoshuhudia makabidhiano hayo amemshukuru Mhe Masala pamoja na kuwaomba ushirikiano watendaji wote wa Ilemela kwa kufanya kazi pamoja ili kuweza kumsaidia Mhe Rais.
"Neno ninalolichukua kutoka kwa Mhe Hassan Masala, ni kwamba hawa wamefanya kazi yangu kuwa rahisi, niwaombe muendelee kuifanya kazi yangu kuwa rahisi, tukafanye kazi pamoja ya kumsaidia Rais Dkt Samia"
Bi Ummy Wayayu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amemshukuru Mhe Masala kwa ushirikiano wake katika kipindi ambacho wamefanya nae kazi kwa takriban mwaka mmoja.Huku akimkaribisha Mhe Mkalipa na kumuahidi ushirikiano wa kutosha
"Nikushukuru kiongozi tumefanya kazi nzuri sana kwa karibu na kwa ushirikiano mkubwa,kwako Mhe mkalipa nikukaribishe Ilemela, tuna imani pale alipoachia Mhe Masala basi utashika kijiti kwenda mbele zaidi ya pale alipoishia yeye nikiwa na imani kubwa kuwa kupitia uongozi wako tutakwenda vizuri zaidi", amesema Bi Ummy
Hassan Millanga ambae ni katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela, akimuelezea Mhe Masala amesema kuwa Mhe Masala ni kiongozi mshirikishaji siku zote madirisha yake yalikuwa wazi kwa chama ambapo akatumia wasaa huo kumshukuru Mungu kwa kumpata mtu mwema, mambo ambayo huwa hayatokei mara kwa mara na kumuahidi Mhe Mkalipa kumpa ushirikiano wa kutosha.
Takribani wiki tatu zimepita toka Mhe Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipofanya mabadiliko na uteuzi wa viongozi mbalimbali, na Wilaya ya Ilemela ni miongoni mwa wilaya zilizoguswa na mabadiliko hayo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.