"Ardhi yote inapaswa kupangiwa matumizi bora kulingana na eneo na shughuli inayokusudiwa kutekelezwa katika eneo husika.Ujenzi wa shule uzingatie mpangilio mzuri wa miundo mbinu yake ili kuleta mvuto sambamba na kuweka vitu vingi zaidi vyenye tija kwa kutumia eneo linalotosheleza . "
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Ilemela Mhe.Angeline Mabula ambaye pia ni Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi wakati wa ziara ya ukaguzi na kutembelea miradi ya Boost ambayo inahusisha ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na awali ambapo Manispaa ya Ilemela ilipokea jumla ya shilingi Bilioni 1.57 kutoka serikali kuu kupitia mradi wa BOOST .
Katika ziara hiyo Mhe.Mabula amewataka wataalam na wananchi wote kwenye maeneo ya miradi ya maendeleo inakotekelezwa kuwa waadilifu katika matumizi ya fedha na kubeba umiliki wa miradi yote na kuzingatia nguvu ya utatu katika utendaji wao ambapo wananchi ,serikali na Mbunge wanapaswa kuwa wamoja ili kufanikisha malengo waliojiwekea kwa wakati.
Aidha Mhe.Mabula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali huku akifafanua kuwa zaidi ya shilingi Bilioni 50 zimepokelewa katika wilaya ya Ilemela kutoka serikali kuu ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Mhe.Samia.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Masala ametoa pongezi kwa timu nzima ya uongozi na wataalam wa Ilemela walioshiriki tangu mwanzo wa zoezi la usimamizi wa miradi hiyo inayoendelea hadi hatua iliyofikia sasa na kuwasihi kuendeleza ushirikiano .
Madiwani kutoka kata za Kahama na Buswelu kwa niaba ya wananchi wao, ambapo shule mpya za msingi zinajengwa kupitia mradi wa BOOST wamemshukuru Mhe. Samia kwa fedha kiasi cha Shilingi Milioni 540.3 kwa kila shule kwani shule hizo zinaenda kuondoa changamoto ya wanafunzi ya kutembea umbali mrefu kwenda kufuata elimu na kusema kuwa lilikuwa hitaji la muda mrefu katika maeneo hayo shule zinapojengwa
Miradi mingine iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa bweni kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum na zahanati ya Lumala.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.