Mhe Jenista Mhagama (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora ametoa maelekezo kwa uongozi wa Ilemela kuhakikisha kuwa miradi yote ya TASAF inakamilika.
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi aliyofanya akikagua utekelezaji wa miradi ya TASAF III katika wilaya ya Ilemela, ambapo amekagua mradi wa ujenzi wa zahanati ya mihama pamoja na nyumba ya mtumishi.
“Miradi hii ikamilike haraka sana kwani mifumo imefunguka, fedha zipo na wananchi wapo, na miradi hii kumi itakapokamilika , naomba kuahidi kuwa tutaleta miradi mingine kumi kupitia fedha hizi za OPEC chini ya TASAF” ,Mhe Mhagama
Mhe Mhagama ameongeza kusema kuwa itakapofika mwezi wa nne ni lazima turudi hapa tuanze kuona zahanati hii inaanza kazi hatuna haja ya kuchelewesha miradi hii mikubwa hasa hii inayojibu kero na mahitaji makubwa ya wananchi wetu na hasa akina mama, watoto na wazee hivyo tuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa miradi hii inakamilika mapema.
Kuhusu malalamiko juu ya walengwa wa TASAF wasiokuwa na sifa, amewaeleza walengwa hao kuwa jambo hilo la mtu ambae hana sifa lipo mikononi mwao, utaratibu wa kumchagua mwenye sifa unafanyika kwenye mitaa yao, pamoja na hayo akatoa maelekezo kwa uongozi wa Ilemela kuanza kufanya mikutano katika mitaa kwa ajili ya kufanya tathmini ya walengwa wa TASAF.
“Fedha hizi anatakiwa apate mlengwa ambae anazingatia vigezo, na kila mtu akimuona aone kuwa anastahili kutunzwa na mfuko wa TASAF hivyo nikuombe Mhe. DC usimamie swala hili”, Mhe Mhagama
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amemhakikishia Waziri Mhagama kukamilisha Ujenzi wa Zahanati na Nyumba ya mtumishi kwenye mtaa wa Mihama ili wananchi waanze kupata huduma za afya kufikia Machi 28, 2023 hasa kwa huduma za afya ya Mama na Mtoto na Lishe.
Vilevile, Mhe. Hassan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwaletea Miradi ya TASAF wananchi wa Kata ya Kitangiri huku akibainisha kuwa imeendelea kuleta chachu kwenye maendeleo na amewapongeza wanannchi wa kata hiyo hasa wa Mitaa ya Jiwe Kuu na Mihama kwani awali wananchi walikua na kiu ya kupata zahanati kwenye eneo lao.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi wa Kitangiri hususan mitaa ya mihama na jiwe kuu , Diwani wa kata ya Kitangiri Mhe. Donald Protas, amesema kuwa TASAF imeweka historia kwenye kata yao kwani imesababisha kuanza kwa maendeleo ya kasi katika sekta ya afya , huku akiwashukuru na kuwapongeza wananchi wa mitaa hiyo kwa namna ambavyo wamejitolea kuhakikisha zahanati hiyo inajengwa .
Leonard Robert mratibu wa TASAF ilemela, katika taarifa yake amesema kuwa kukamilika kwa mradi huu ambao unatarajiwa kugharimu takriban kiasi cha shilingi milioni 219. 25, kutasaidia kusogeza huduma ya afya ya uzazi, maendeleo ya mtoto na lishe karibu zaidi na wananchi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.