Mhandisi Modest Joseph Apolinary aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe: Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 01/08/2021 kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amekabidhiwa ofisi rasmi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hii Ndugu John Paul Wanga leo tarehe 09/08/2021.
Makabidhiano hayo yamefanyika mbele ya Kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya ya Ilemela, Mstahiki meya na baadhi ya Waheshimiwa madiwani, pamoja na wakuu wa Idara wa Manispaa hii ambapo Ndugu Wanga amemkabidhi nyaraka na taarifa muhimu kuhusiana na Manispaa ya Ilemela ikiwemo Ilani ya CCM.
Mara baada ya makabidhiano hayo Mkurugenzi anaendoka alipata wasaa wa kuwaaga watumishi wa makao makuu na kuwahimiza kutoa ushirikiano kwa mkurugenzi mpya kwa kufanya kazi kwa uadilifu na ueledi huku akiwashukuru kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote alichokuwepo katika Manispaa hii ya Ilemela.
Pamoja na hayo amemsihi Mhandisi Apolinary kuendeleza yale mazuri aliyoyaacha ikiwa ni pamoja na kuleta matokeo chanya ambayo yatapelekea kuwa na Ilemela yenye maendeleo.
Kwa niaba ya watumishi wa Manispaa ya Ilemela Ndugu Marco Busungu (Afisa Elimu Msingi), na Ndugu Neema semwaiko(Afisa Kilimo) kwa nyakati tofauti waliahidi ushirikiano kwa Ndugu apolinary, na kumtakia kila la kheri Ndugu Wanga kwa kusema kuwa alikuwa ni mwalimu mzuri kwa watumishi aliowangoza.
Katibu Tawala Ndugu Said Kitinga akiwakilisha kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ilemela alimuahidi Ndugu Apolinary ushirikiano wa kutosha kwani wanajenga nyumba moja huku akimhimiza Mkurugenzi wanga kuwa akaitangaze vyema Ilemela kwa kuendeleza mazuri yake huko anapoenda.
Mhe. Renatus Mulunga ambae ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela alisema kuwa anaamini utendaji wa Mkurugenzi Wanga na kumuahidi Mkurugenzi Apolinary ushirikiano katika kipindi chote atakachokuwepo Ilemela huku akiwasisitiza watumishi wote kuwa kila mmoja asimame katika nafasi yake na kutekeleza majukumu yao.
Mhandisi Modest Apolinary anakuwa ni mkurugenzi wa 3 tangu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuanzishwa mwaka 2012 nae amewaomba watumishi ushirikiano ili kuweza kuzitatua changamoto mbalimbali katika Manispaa hii ya Ilemela hususan za wananchi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.