Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathew ameleta matumaini ya upatikanaji wa maji katika maeneo yote ya Wilaya ya Ilemela.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara kusikiliza kero za maji uliofanyika viwanja vya shule ya msingi Buswelu Mhe . Kundo amesema upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi ni moja ya kipaumbele cha serikali ya awamu ya sita.
" Upatikanaji wa maji safi na salama ni kipaumbele chetu kwa kuanzia maeneo yote ya umma. Mhe. Rais anataka wananchi wake wote wapate maji na mimi sitakubali kumkwamisha . "
Ameitaka mamlaka ya maji Mwanza ( MWAUWASA ) kuhakikisha maji yanapatikana maeneo yote yenye miundo mbinu rafiki na kuwataka wataalam wake kuendelea kusambaza na kufukia mabomba kwa wakati ili kuepuka uharibifu wake.
Akijibu hoja ya Dominic Thomas mkazi wa mtaa wa Nyamadoke kata ya Nyamhongolo kuhusu suala la wananchi kununua vifaa vya kuunganishia maji MWAUWASA tu na si sehemu nyingine Mhe. Kundo ametoa maelekezo kwa wananchi kupata muongozo wa aina "specification" ya vifaa vya ubora unaohitajika kutoka kwa wataalam wa MWAUWASA na kununua vifaa hivyo popote huku akiwasihi kuacha kazi ya kufunga vifaa hivyo iwe ya mafundi wataalam kutoka MWAUWASA.
" Wananchi ombeni kuunganishiwa maji kwa maandishi,kazi ya kuunganisha ni ya fundi na nyinyi msiwe mafundi muache fundi afanye kazi yake akiharibu tupate wa kumuwajibisha."
Aidha amewataka wananchi kutunza , kulinda mita na miundo mbinu yote ya maji huku akiwasihi MWAUWASA kuanza kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuwa na miundo mbinu kuanzia kwenye vyanzo vya maji hadi kumfikia mtumiaji.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Bi. Nelly Msuya amesema zaidi ya wananchi 340 wa Ilemela wameunganishiwa huduma hiyo na kukiri kusimama kwa zoezi hilo kutokana na kuisha kwa vifaa vya kuunganishia huku akiahidi vifaa kupatikana mwezi Agosti 2024 na zoezi kuendelea mara moja.
Mhe. Sarah Ng'hwani ni diwani wa kata ya Buswelu anamshukuru Mbunge wa Ilemela Mhe.Dkt. Angeline Mabula kwa kupokea kero mbalimbali na kuzifikisha bungeni ambako zinafanyiwa kazi kwa wakati.
Akihitimisha mkutano huo Mhe. Mabula ameunga mkono juhudi za kumtua mama ndoo kichwani huku akimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha nyingi jimboni mwake kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.