Mgogoro wa ardhi katika eneo la Kigoto kata ya Kirumba uliodumu muda mrefu kwa zaidi ya miaka thelathini iliyopita umehitimishwa rasmi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe. William Lukuvi alipogawa ankara za malipo kwa wananchi wa eneo hilo la Kigoto.
Waziri Lukuvi akihutubia wananchi wa kigoto amesema kuwa amekuja kuhitimisha mgogoro huo rasmi kwa kuwakabidhi wananchi hao ankara za malipo ili waweze kuandaliwa hati ya miaka 99 na hii ikiwa ni baada ya uamuzi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuagiza kuwa wananchi hao wamilikshwe ardhi.
Aliongeza kwa kusema kuwa jumla ekari 56 za serikali zimetolewa kwa wananchi wa eneo la Kigoto huku jumla ya ekari 16 zikiwa zimebaki katika Jeshi la polisi kwa kufuata maelekezo ya Mhe. Rais.
Akigawa ankara hizo za viwanja 600 kwa wananchi wa Kigoto, ameitaka Idara ya ardhi kuhakikisha kuwa mwananchi anapolipia gharama za umilikishaji anapatiwa hati yake ndani ya siku 7.
Aidha amewahimiza wananchi kuhakikisha wanafanya malipo yaliyoainishwa katika ankara za malipo ili waweze kupatiwa hati na amesema kuwa angefurahi iwapo wananchi wote ndani ya miezi 3 wawe wamelipia na kumiliki hati zao ili ziweze kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.
Akifikisha salam za Mhe. Rais na kusema kuwa, Rais Magufuli amewataka wananchi wa eneo hilo kuondoa hofu kwani eneo hilo la serikali la ukubwa wa ekari 56 limetolewa bure kwa wananchi, na gharama zitakuwa ni kwa ajili ya kulipia umilikishwaji tu na si vinginevyo.
Pamoja na hayo Waziri Lukuvi amewataka wananchi kuacha kuvamia maeneo ya serikali kwa kudhani kuwa watakuja kumilikishwa na kuzitaka taasisi zote za serikali kuhakikisha wayalinda maeneo yao yasivamiwe kwani ni jukumu lao.
Nae Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe Angeline Mabula amemshukuru Mhe. Rais kwa kutatua mgogoro huu uliokuwa ukileta adha kubwa kwa wananchi kwani wananchi walishindwa kupata huduma mbalimbali za kijamii
Kupitia wananchi wa Kigoto Mhe Mbunge amewaahidi wananchi wa Ilemela kuwa atahakikisha changamoto za migogoro ya ardhi zinatatuliwa na kuisha kabisa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, amemshukuru Rais kwa kitendo chake cha kuwajali wanyonge na kusema kuwa kitendo cha kuwapa bure wananchi ekari 56 inaonyesha ni namna gani Rais anawajali wananchi wanyonge.
“Ekari 16 zimebaki kwa jeshi la polisi huku ekari 56 zikienda kwa wananchi, hali hii inadhihirisha kuwa Mhe. Rais anatetea wananchi wanyonge”, Alisema.
Mgogoro huu uliohusisha jeshi la polisi na wananchi ulianza kutatuliwa na serikali kuanzia mwaka 2017 ambapo ulipitia katika hatua mbalimbali chini ya Wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.