Ndugu Charles Marwa ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela amewataka wadau mbalimbali kujitokeza na kuendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika shughuli za kimaendeleo hata bila ya kuombwa.
Rai hiyo ameitoa alipokuwa akipokea vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Shirika lisilo la kiserikali la SOS Children’s Village Tanzania linalojishughulisha na malezi ya watoto kwa ajili ya kuimarisha sekta za Afya na Elimu katika Manispaa ya Ilemela.
Nae Mama Doroth Ndege ambae ni Meneja mradi wa shirika hilo Mkoani Mwanza amesema kuwa jumla ya shilingi Milioni 50,875,500 imetumika katika manunuzi ya vifaa hivyo vinavyotarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 472,800 wanaopatiwa huduma ya afya katika vituo vya kutolea huduma ya afya huku upatikanaji wa vitabu vya ziada na kiada kunufaisha wanafunzi 1093 ndani ya Manispaa ya Ilemela.
Mkurugenzi wa shirika la SOS Children’s village Tanzania ndugu David Mlongo amesema shirika lake litaendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kuleta maendeleo maeneo yote ambako shirika linafanya kazi zake nchini.
“SOS Children’s village Tanzania ni shirika linalojali maendeleo kuanzia ngazi ya familia kupitia malezi ya watoto, na ni wadau wakubwa wa maendeleo katika mkoa huu wa Mwanza, tunashukuru kwa kupokelewa vizuri katika wilaya hii ya Ilemela na shughuli zetu zimekuwa za kuzaa matunda tunayoyakusudia hivyo nasi hatuna budi kurudisha katika jamii ndio maana leo hii tumeamua kuunga mkono juhudi za maendeleo katika Manispaa ya Ilemela”. Alisema
Aidha Mkurugenzi Mlongo mbali na kuelezea fursa mbalimbali zinazotolewa na shirika lake ikiwemo kutoa elimu na kuziwezesha familia kiuchumi ili walezi waweze kutoa huduma ipasavyo kwa watoto walio katika mazingira magumu pamoja na vijana waweze kufikia ndoto zao akatumia fursa hiyo kuwataka wananchi na wadau wengine kuendelea kuungana pamoja ili kupambana na maadui wakuu wa tatu wa tangu kipindi cha uhuru kwa maana ya ujinga, umasikini na maradhi.
Mganga Mkuu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amemshukuru Mkurugenzi wa SOS na kuupongeza uongozi mzima wa shirika hilo kwa jitihada zao za kuhamasisha wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo asasi zisizo za kiserikali huku akiahidi kutumia vizuri vifaa vyote vilivyotolewa ili vikatekeleze lengo lililokusudiwa
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja dawa za kuongeza damu( Fefo 200mg) boksi 990,gloves boksi 250,gauze absorbent rola 100,vifaa mbalimbali vya steshenari kama karatasi za kuandikia “ream paper”,mashine ya kutolea kopi pamoja na vitabu vya ziada na kiada ambapo vitabu vya shule ya msingi pisi 551 vimetolewa na vya sekondari pisi 574.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.