Mwaka 2022 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilianza kutumia mfumo wa E-Board lengo ikiwa ni kurahisisha uendeshaji wa vikao na kupunguza gharama za maandalizi ya vikao hivyo.
Mfumo wa E- Board ambao umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) hutumika kuwezesha uratibu wa shughuli za uandaaji wa vikao mbalimbali vya bodi na menejimenti katika Halmashauri na Taasisi za Umma .
Kuanza kutumika kwa mfumo huu wa E-Board katika Manispaa ya Ilemela kumesaidia kuokoa matumizi ya fedha nyingi zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya manunuzi ya shajara, wino na vifaa vingine kwa ajili ya maandalizi ya vikao ikiwemo kudurufu taarifa mbalimbali kwani kwa sasa taarifa hizo zinapakiwa kwenye mfumo na kisha madiwani na wataalam wamekuwa wakipakua kwa ajili ya kuzifanyia kazi, amefafanua Bi Ummy Wayayu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela.
“Kwa mwaka tulikuwa tunatumia takribani shilingi milioni 200 hadi 300 kuandaa vikao, lakini kwa sasa gharama hizo hatuna tena kwani tunatumia mfumo huu wa e-Board, ambao umesaidia kupeleka fedha hizo katika mambo mengine ya muhimu ya halmashauri,” alisema Bi.Ummy.
Mkurugenzi Ummy ameongeza kusema kuwa mfumo wa e-Board umeweza kuwasaidia madiwani kupokea taarifa ya kikao hata wanapokuwa nje ya halmashauri hiyo kupitia vishkwambi ambavyo wamewezeshwa kwa ajili ya matumizi ya mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuweza kujua agenda za vikao na kufuatilia yatokanayo ya vikao na hivyo umeweza kuokoa muda wa kuendesha vikao vya halmashauri.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mheshimiwa Renatus Mulunga, amesema kuwa mfumo wa e-Board umewasaidia madiwani kuendesha vikao vyao kwa ufanisi ili kuboresha huduma za wananchi wa Ilemela. Na hivyo kutoa rai kwa halmashauri nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo wa e-Board, kufanya ziara halmashauri ya Manispaa ya ilemela ili kuweza kujifunza au kuwasiliana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ili zipate uelewa kuhusu mfumo huo.
Sara Lisso ni Diwani wa viti maalum yeye amepongeza matumizi ya mfumo huu kwani ni rahisi kutumia na popote ulipo unaweza kusoma kikao husika , pamoja na hilo kupitia mfumo wa E-Board umewawezesha madiwani kujihudhurisha kwenye kikao au kuomba udhuru wa kikao popote pale anapokwepo.
Kupitia mfumo huu wa E-board umesaidia kuokoa muda wa kusambaza makabrasha kwani hapo awali ilibidi kuhakikisha makabrasha ya vikao yanasambazwa kwa madiwani katika kata zote 19 za Halmashauri. hayo yamebainishwa na Mwandishi wa Vikao Ndugu Shilinde Malyagili.
Tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa E-Board takribani vikao 50 vimeendeshwa vikao hivyo vimejumuisha vya menejimenti , vya kamati za kudumu na vikao vya baraza la madiwani.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.