Mbuzi 424, wa thamani ya shilingi milioni 36.04 wametolewa kwa kwa kaya 106 zinazonufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF kupitia mradi wa kuongeza kipato unaofadhiliwa na OPEC.
Pamoja na kukabidhiwa mbuzi hao, walengwa wa TASAF wametakiwa kuupokea mradi huo kwa mikono miwili sambamba na kuhakikisha wanawatunza mbuzi hao ili waweze kuzaliana na baadae waje kuwasaidia katika utatuzi wa changamoto za kiuchumi katika kaya zao ikiwa ndio lengo la mradi huu.
Rai hiyo imetolewa na Ndugu leonard Robert ambae ni mratibu wa TASAF Ilemela, na kuongeza kusema kuwa anayo matarajio makubwa kuwa uchumi wa kaya unaenda kuimarika kupitia mradi huu.
“Matarajio makubwa ni kwamba uchumi wa kaya unaenda kuimarika na changamoto zinaenda kupungua ambapo kila kaya itakuwa na jukumu la kuwatunza na kuwalinda, tunaamini mradi huu unaenda kutatua changamoto za kiuchumi ndani ya familia”, amesema Ndugu Leonard
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Bi Suzana Tilumanywa amewataka wanufaika wa mradi huo pamoja na uongozi wa kata na mtaa kuhakikisha wanaulinda mradi huo na kuutunza ili tija iliyokusudiwa iweze kufikiwa pamoja na kushauri wataalam wa wilaya wakiwemo na maafisa mifugo kufuatilia changamoto za walengwa hao na kuzipatia ufumbuzi.
‘.. Ilemela tumekuwa wa kwanza kutekeleza mradi huu, Tukifanya vizuri wenzetu wa maeneo mengine watakuja kujifunza kutoka kwetu ..’ Alisema
Nae Diwani wa kata ya Nyamhongolo Mhe Andrea Nginila amefafanua kuwa mradi huo utaenda kuleta tija kwa wananchi wake kwa kuwaondolea umasikini kwa kuwa utawazalishia fedha za kujikimu wao binafsi na wategemezi wao
Leah Mabula ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ambapo ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha hizo na kuahidi kutunza mbuzi hao waweze kuzaliana ili familia yake iweze kujikomboa kiuchumi
Mbuzi hawa wametolewa kwa mitaa miwili ya kata za Sangabuye na Nyamhongolo ambapo mtaa wa Igalagala uliopo kata ya Sangabuye wamepata mbuzi 196 na mtaa wa Ibinza katika kata ya Nyamhongolo wamepatiwa mbuzi 228 ambapo kila kaya imepatiwa mbuzi wanne kati yao watatu ni majike na mmoja ni dume .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.