Mbunge wa jimbo la Ilemela, Mhe Dkt Angeline Mabula, leo tarehe 24.01.2019 amekabidhi jumla ya mifuko ya saruji 700 na mifuko 1200 ya chokaa kwa uongozi wa Manispaa ya Ilemela.
Akikabidhi saruji na chokaa hiyo kwa uongozi wa Manispaa ya Ilemela , katibu wa Mbunge kwa niaba yake Mbunge amesema kuwa Mhe Mbunge ameelekeza kuwa saruji na chokaa hiyo itumike katika ujenzi wa madarasa ya Shule za sekondari Ilemela kwani upungufu wa madarasa ni mkubwa kutokana na ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba 2018.
Pamoja na hayo Mbunge ametoa shukrani za kipekee kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martine Shigela kwa ushirikiano wake mkubwa katika kufanikisha kupata msaada huo, pia ameishukuru kampuni ya usafirishaji ya Z.B MINING LTD kwa kusafirisha saruji na chokaa hiyo.
Ndugu Jonex Joel, mwakilishi kutoka kampuni ya TEXAS ambae ni wakala kwa kanda ya ziwa amesema kuwa, ufadhili huo umetolewa ikiwa ni katika kuunga juhudi za Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mhe Mbunge wa Jimbo la Ilemela katika kuwaletea maendeleo wananchi.
“Tumeona upo umuhimu wa kuunga juhudi za Mbunge kwani amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta misaada mbalimbali kwa ajili ya wananchi wa Ilemela pia tunawakaribisha kuleta maombi mengine kama lipo ndani ya uwezo wetu tutatoa”, Alisema
Mstahiki Meya wa Ilemela, Mhe.Renatus Mulunga nae amemshukuru Mbunge kwa jitihada zake mbalimbali katika kutatua changamoto katika jimbo la Ilemela,kwani mbali na kutafuta saruji na chokaa amekuwa ni msaada mkubwa kwa kutoa matofali kwa ajili ya ujenzi wa maboma kwa shule za Ilemela.
“Ukitaka nchi iendelee wekeza kwenye elimu, na dhamira kuu ni kutaka kuona Ilemela inatoka hapa ilipo na ndio maana Ilemela inatumia njia ya ushirikishaji kuanzia ngazi ya jamii ambapo wananchi wanajenga msingi, mbunge anajenga boma kwa kutoa matofali na kisha Manispaa inakamilisha jengo kwa kuezeka”, alisema
Nae Ndugu John Wanga, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, amesema kuwa saruji na chokaa ina manufaa makubwa katika kukabiliana na changamoto ya ujenzi wa madarasa na hili limetokana na ufaulu mkubwa Ilemela kwa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka 2018.
Aidha aliongeza kwa kusema kuwa, Mbunge ameendelea kutembea na kauli mbiu , “mrithishe elimu mtoto na sio mali”, kwa kuhakikisha kuwa madarasa yanakamilika na kwa jitihada hizi atatimiza ndoto ya kuwekeza elimu kwa mtoto.
Mifuko 700 ya saruji imefadhiliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Cement na Kampuni ya Neelkanch Chemical Ltd imetoa mifuko 1200 ya chokaa ikiwa ni jitihada za Mbunge wa Ilemela katika kutatua changamoto za ujenzi wa madarasa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.