MBUNGE WA ILEMELA KUKUZA NA KUENDELEZA VIPAJI VYA MICHEZO ILEMELA
Mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe. Angeline Mabula amezihakikishia timu za Manispaa za Ilemela kwa shule za msingi na sekondari kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali vya michezo vilivyomo ndani ya jimbo lake.
Mhe mbunge aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kupokea kombe la ushindi wa michezo ya UMITASHUMTA yaliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya bwiru ambapo timu ya wilaya ya Ilemela ilishika nafasi ya kwanza kimkoa.
Aidha aliwahakikishia kuwa michezo inakuwa fursa ya kujikomboa kichumi kwa kuifanya ajira kama ajira nyingine kwa kuwalea,kuwasomesha pamoja na kuwatafutia ufadhili mbalimbali ili michezo ikawe daraja la kuwapandisha vijana ambao wana kipaji vya michezo.Katika kulitekeleza hilo ameahidi yeye pamoja na Tanzania football House kuwalea wanafunzi wawili walionyesha vipaji vyao katika michezo.
“Mimi pamoja na Tanzania Football house tutawalea,tutawasomesha na kuwatafutia ufadhili ili iwe chachu kwa wale ambao hawakupata fursa hii ili michezo ikawe sehemu ya kuweka afya zetu sawa pamoja na kuwa daraja la kumpandisha daraja kijana mwenye kipaji”, alisisitiza.
Pamoja na hayo aliipongeza na kuishukuru timu hiyo kwa kuwa mabalozi wazuri kwa ilemela, na kusema kuwa ushindi huu umeletwa na wao kuwa wasikivu kwa walimu wao pamoja na nguvu ya pamoja kutoka ofisi ya Mbunge kupitia taasisi ya Angeline, ofisi ya mkurugenzi, walimu, wazazi na Tanzania football house.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela akiwapongeza vijana hao aliwataka kuchangamkia fursa ya kubadilishana uzoefu na nchi ya Korea Kusini pindi itakapotokea ambayo kwa sasa imeanzisha mahusiano na Manispaa ya Ilemela kwa kuongeza bidii katika michezo .Pamoja na hayo aliwataka kuzingatia masomo yao kwa kusoma kwa bidii, halikadhalika alimshukuru Mbunge kwa juhudi anazofanya katika kunyanyua michezo Ilemela kwani hilo ni jukumu la baraza la madiwani.
Mashindano hayo ya UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa yalianza tarehe 8/06/2017 na kuhitimishwa tarehe 12/06/2017 huku timu ya ilemela ikishika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Misungwi na nafasi ya tatu kushikwa na Buchosa.Kumalizika kwa mashindano hayo kumewapa fursa wanafunzi 15 kutoka timu ya Ilemela kuungana na timu ya Mkoa wa Mwanza kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA kitaifa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.