Wananchi wanaopimiwa viwanja na kisha upimaji ukaidhinishwa wametakiwa kutokwepa kumilikishwa ardhi, kwani kufanya hivyo ni kutenda kosa kisheria.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa zoezi la ugawaji wa hati 1300 kwa wananchi wa manispaa ya Ilemela, mbapo amesema kuwa ipo tabia kwa baadhi ya wananchi kuomba kupimiwa viwanja vyao na baada ya hapo kukwepa kulipa kodi kwa kukataa kuomba kumilikishwa maeneo yao kitendo ambacho kimekuwa kinaikosesha Serikali mapato.
Aidha Dkt Mabula aliwahimiza wananchi kutumia fursa hii ya urasimishaji kwani zoezi hili si endelevu na halina fidia kwa kuwa limetokana na msamaha wa Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa wananchi wake baada ya kuona wamejenga bila kufuata utaratibu hivyo kuamua kuwarasimishia makazi yao ili waishi kwa amani na utulivu bila ghasia yoyote ikiwemo kuvunjiwa.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Kamishna wa ardhi mkoa wa Mwanza Ndugu Makwasa Musase Biswalo amesema kuwa zoezi la ugawaji hati kwa wananchi litakuwa likiendeshwa kwa kuwafata wananchi katika maeneo yao badala ya kuwasumbua kwa kila siku kuzifuata katika ofisi za ardhi za mkoa na halmashauri ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya wizara huku akimshukuru Naibu Waziri huyo kwa ushirikiano anaotoa kwa ofisi yake.
Bwana Julius Peter ni moja ya wananchi waliokabidhiwa hati miliki katika zoezi hilo ambapo ameishukuru Serikali kwa kuruhusu zoezi la urasimishaji makazi na kuwataka wananchi wengine kutumia fursa hiyo kikamilifu
Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, imepanga kuandaa hati 5000 na hadi sasa zimeshaandaliwa hati 327 kati ya hizo hati 96 ni za mradi wa viwanja vya walimu na 231 ni hati za maeneo mengine’Hayo yalisemwa na Bi grace Masawe ambae ni afisa ardhi mteule wa Manispaa ya Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.