Katika kutekeleza agizo la serikali kwa kila Halmashauri la kutoa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha vikundi vya wanawake asilimia 4,vijana asilimia 4 na watu wenye ulemavu asilimia 2, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia Idara ya Maendeleo ya jamii imeendesha mafunzo ya mikopo kwa vikundi ambavyo vitapatiwa mkopo.
Mafunzo hayo yametolewa kwa awamu na wataalam wa maendeleo ya jamii kwa vikundi takribani 70 lengo ikiwa ni kuwakumbusha malengo ya serikali katika utoaji wa mikopo bila riba ,kufundishwa kanuni na sheria mbalimbali juu ya mikopo sambamba na elimu ya ujazaji wa mikataba .
Wakati wa mafunzo hayo Mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii Ndugu Sitta Singibala ametoa rai kwa vikundi vyote vinavyopata mikopo kutumia kwa malengo ili waweze kurejesha kwa wakati kuepuka usumbufu wa kudaiwa kwa nguvu hadi kwenye vyombo vya sheria, kitu kinachopoteza muda wa kuzalisha na kuminya fursa za wanajamii wengine kupata mkopo.
“Ni muhimu fedha ziwekwe kwenye mzunguko wa biashara au shughuli ya kuzalisha yenye kuingiza fedha ili kurahisisha zoezi la urejeshaji fedha za mkopo”alisema Sitta Singibala.
Aidha Afisa Maendeleo msaidizi Bi.Florence Vedasto amesisititiza wanavikundi kufata taratibu za kifedha katika kurejesha mikopo yao. “Kufata taratibu za kurejesha mikopo ni lazima kwani zoezi linakuwa katika mfumo mzuri na wa kueleweka.Akaunti ya kutumia ni 0150478109500 ya benki ya CRDB.Mkumbuke baada ya kupata slipu ya benki mnaileta Manispaa ili kupata risiti nyingine ya kuthibitisha marejesho yako yamepokelewa.”
Akiongezea wakati wa mafunzo hayo Afisa maendeleo ya jamii Bi.Amina Bululu amesema ni lazima vikundi kufanya kazi kwa malengo na bidii ili tija ya watu kuwa pamoja ionekane.
“Ni wakati wa vikundi kufanya kazi kama kikundi kweli na sio maigizo.Ni muhimu kuwa na miradi ya pamoja ili kupata matokeo makubwa na ya pamoja katika kuleta maana halisi ya vikundi.”
Akihitimisha mafunzo hayo Afisa vijana wa Manispaa ya Ilemela Bi.Lucy Matemba amewataka wanavikundi hao hasahas vikundi vya vijana kuzingatia umri wao.Umri wa kijana ni kuanzia miaka 18 hadi 35 kwa mujibu sheria ya Tanzania
“Ukiona umri wako umezidi jitoe au omba kuwa mlezi wa kikundi ili wengine wenye umri husika wapate nafasi ya kujiunga.Tunataka mikopo hii izae matunda chanya ya kusika Tanzania nzima,msisite kuuliza kwetu mnapokwama.Tupo kwa ajili yenu”
Manispaa ya Ilemela inatarajia kutoa jumla ya shilingi Milioni 197 kwa vikundi 77 vinavyojumuisha vikundi vya wanawake 59, vijana 15 na vikundi vya watu wenye ulemavu vitatu ndani ya Wilaya ya Ilemela kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi machi 2020
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.