Na Violencea Mbakile- IlemelaMc
“Maendeleo endelevu yanatokana na sisi wenyewe kumiliki miradi tunayoletewa na ile ambayo tumeshiriki bila ushiriki wetu hatuwezi kuona nini kinaendelea kwa hiyo hiki tulichokifanya hapa iwe ni muendelezo katika miradi yetu”,Mhe Dkt. Mabula
Mhe. Dkt Angeline Mabula, ambae ni Mbunge wa jimbo la Ilemela na Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi wa Ilemela mara baada ya uzinduzi wa majengo mawili ya mama na mtoto katika zahanati za Ilemela na Nyakato pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo la wodi ya wazazi lililopo kituo cha Afya Buzuruga.
“Sidhani kama mtakubali mtu achezee miundombinu hii kwani nguvu yako iko hapo na hii ndio maana halisi ya maendeleo endelevu yanayotokana na sisi wenyewe kumiliki miradi tunayoletewa na ile ambayo tumeshiriki” Amesema Mhe Mabula
Pamoja na hayo amewapongeza wananchi wa Ilemela kwa namna ambayo wamekuwa wakishiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo huku akitolea mfano namna ambavyo wananchi wa kata ya Nyakato wameweza kuchangia kiasi cha Tshs. Milioni 10.4 katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati ya Nyakato na kusema kuwa kazi kubwa imefanyika.
“Nawapongeza sana wananchi, milioni 10.4 kutoka kwa wananchi ni kazi kubwa imefanyika na haya ndio Mhe Rais anayataka, hataki maneno maneno anataka kazi ifanyike hapo kuna mkono wa wananchi, mbunge na serikali tunapounganisha nguvu siku zote mambo lazima yaende mbele na unapotaka kupika ili chakula kiive lazima uwe na mafiga matatu katika maendeleo na katika majengo ya mama na mtoto haya hapa tumeenda na mafiga matatu yaani wananchi, Mbunge na Halmashauri” amesema akiwapongeza wananchi
Mhe. Dkt Angeline Mabula ametumia hadhara hiyo kumpngeza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kwa ubunifu wake ambao umeongeza kasi ya maendeleo katika sekta zote na kusisitiza kuendelea na umoja huu kwa kuwashirikisha wananchi kwani wameshafahamu elimu ya kujitegemea na kwasababu wanajua kuwa Mhe.Rais yupo tayari kuhakikisha kwamba nguvu ya wananchi haipotei.
“Mhe.Mkuu wa Wilaya sina shaka na wewe na timu yako na tuendelee na umoja huu tukiwashirikisha wananchi wetu kinachonifurahisha ni ushiriki wa wananchi kwa sababu wamefahamu elimu ya kujitegemea na kwasababu wanajua kuwa Mhe.Rais yupo tayari kuhakikisha kwamba nguvu ya wananchi haipotei sasa tuonyeshe mfano kwa kuongeza kasi ya kujitegemea kwa kuweka miundombinu ya vyumba vya madarasa kwa watoto wa shule za msingi kuondoa msongamano darasani”, amesema Mbunge Mabula
Ndugu Aziza Isimbula, Katibu wa CCM Wilaya ya Ilemela amesisitiza kuhusu kuendeleza ushirikiano uliopo wa wananchi, ofisi ya mbunge na mkurugenzi ili masuala ya maendeleo yazidi kuwa mepesi ambapo amewapongeza wananchi kwa kushiriki shughuli za maendeleo kwani wao ni wadau wa kwanza wa miradi ya maendeleo,
Nae Mhandisi Modest Apolinary Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amesema kuwa kupitia chanzo cha mapato ya ndani Manispaa ya Ilemela imetoa takriban kiasi cha Tsh. Milioni 72. 4 kwa ajili ya kukamilisha majengo mawili ya mama na mtoto katika zahanati za Ilemela na Nyakato ambazo zilikuwa zimekaa kwa muda mrefu bila kukamilika huku kiasi cha Tsh. Milioni 50 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la Wodi ya wazazi katika kituo cha Afya Buzuruga ambapo hadi sasa jengo lipo hatua ya boma.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.