Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Ilemela kupitia Baraza la Kata robo ya nne 2022/2023 wamepata fursa ya kuwasilisha changamoto zinazozikabili kata zao zikiwemo za ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa maji na umeme.
Wakiwasilisha changamoto hizo kupitia taarifa za utekelezaji za kata, madiwani hao wametaja ubovu wa barabara katika kata zao kama moja ya changamoto ambayo imekuwa ni ya muda mrefu na kuitaka TARURA kuipatia ufumbuzi wa haraka kwa kuhakikisha wanakamilisha barabara ambazo hazijakamilika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali katika kata zao na kuwaletea maendeleo wananchi wao. Huku wakitoa rai kuwa barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha lami, mawe au zege ili ziweze kudumu kwa muda mrefu
Sambamba na hilo Madiwani hao kwa umoja wao wametoa rai kwa barabara ambazo zipo karibu na shule na taasisi mbalimbali kuhakikisha zinawekewa taa za barabarani za kuongozea magari alama za kuvukia barabara (Zebra cross) ili kuepusha vifo ambavyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara.
Suala la ukosefu wa maji katika kata za Manispaa ya Ilemela ni changamoto nyingine ambayo iliibuliwa kwa wingi na Madiwani hao na kuomba MWAUWASA kuziangalia upya laini za maji au ziwekwe laini mpya kuwezesha upatikanaji wa maji kwa wananchi. Pamoja na hilo wameiomba Idara ya Maji (MWAUWASA) kuzingatia mgao wa maji katika taasisi za shule ili kuwaondolea adha wanafunzi ya kutafuta maji na badala yake watumie muda huo kujisomea.
Kwa upande wa changamoto ya nishati ya Umeme, waheshimiwa madiwani wakijadili hoja hiyo wametoa rai kwa TANESCO kuhakikisha wanafanyia kazi maombi yanayowasilishwa kwao na hivyo kuwakumbusha wanamalizia kazi ya kuweka umeme katika maeneo mbalimbali ambayo hawajakamilisha zoezi hilo.
Changamoto zingine zilizowasilishwa ni pamoja ni za sekta ya afya ikihusisha ukosefu wa zahanati katika baadhi ya kata, kwa upande wa sekta ya elimu hoja iliyoibuliwa ni suala la upungufu wa walimu, madawati kwa baadhi ya shule, ukamilishaji wa miradi viporo ikiwemo ofisi za kata/mitaa, zahanati pamoja na maboma ya shule na kumuomba mkurugenzi kuhakikisha anatatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa miradi ya nyuma
“Ifike wakati sasa miradi iliyoanzishwa ikamilike ili wananchi nao wapate moyo wa kuweza kuchangia maendeleo katika kata zao kwani kwa sasa inakuwa ni vigumu kwenda kuomba wananchi wachangie maendeleo kutokana na kuwa wanaona miradi ya nyuma waliyochangia haijakamilika,”Amesema Diwani kutoka kata ya NyakatO Mhe. Jonathan Mkumba
Akijibu hoja ya kuhusiana na suala la ukamilishaji wa miradi viporo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ndugu Herbert Bilia ambae ni Mchumi wa Manispaa ya Ilemela, amesema kuwa Mkurugenzi amedhamiria kuhakikisha anakamilisha miradi yote iliyoanzishwa hapo nyuma ambapo utekelezaji wake utafanyika kwa awamu mbalimbali kwa kuzipatia kata zote 19 kiasi cha Shilingi Milioni hamsini kwa kuanzia na hivyo kuwataka watendaji wa kata kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani wa kata husika kuhakikisha wanawasilisha orodha ya miradi yote ambayo haijakamilika.
Sambamba na hoja hiyo ya miradi viporo, Ndugu Bilia kwa niaba ya Mkurugenzi amefafanunua kuhusu changamoto iliyoibuliwa ya barabara, amesema kuwa TARURA waliwasilisha bajeti yao katika Baraza la Madiwani hivyo ametoa rai kwa madiwani kuzingatia bajeti iliyowasilishwa na TARURA kwani Serikali inazingatia bajeti iliyopangwa na kuwaomba madiwani kumuunga mkurugenzi juu ya suala la ununuzi wa mitambo ya barabara. Na kwa upande wa changamoto za maji na umeme aliahidi kuwasiliana na mamlaka husika kwa ufumbuzi zaidi.
Akihitimisha kikao hicho Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe Renatus Mulunga amewahimiza madiwani kuhakikisha wanaacha alama hivyo kuwasihi wanafunga mikanda ili kutatua changamoto kata na mitaa huku akiwataka watendaji wa kata kuhakikisha wanakusanya mapato kwa nguvu zote kwani na kila mtu atimize wajibu wake.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.