MADIWANI ILEMELA WAWASILISHA TAARIFA ZA MAENDELEO ZA KATA ZAO
Baraza la madiwani kwa ajili ya kujadili taarifa za kata kwa robo ya kwanza kipindi cha Julai-Septemba 2024/2025, limefanyika leo tarehe 05 Novemba 2024, katika baraza hili madiwani huwasilisha taarifa za maendeleo za kata zao sambamba na changamoto zinazojitokeza katika kata hizo.
Madiwani hawa wa Manispaa ya Ilemela wakiwasilisha taarifa zao katika nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao miradi hiyo ni pamoja na ya sekta ya afya,elimu,maji,miundombinu ya barabara.
Pamoja na shukurani hizo, zipo changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na kubwa ikiwa ubovu wa miundombinu ya barabara likionekana kugusa karibia kila kata ya Manispaa ya Ilemela huku wakiitaka TARURA kufika kwenye kata zao kwa ajili ya kukarabati barabara zilizoharibika. Changamoto nyingine iliyowasilishwa ni suala la fidia, ukosefu wa maji ya uhakika katika baadhi ya maeneo.
Bi Ummy Wayayu ambae ni mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela akijibu hoja hizo zilizoibuliwa ameahidi kufanyia kazi suala la ulipaji wa fidia na kusema kuwa fidia inalipwa kutokana na makusanyo ya fedha za mapato ya ndani.Aidha amewasihi Madiwani kuwa na uvumilivu kwani mitambo ya barabara ipo njiani kufika ambayo itaenda kupunguza changamoto hizo.
Akihitimisha baraza hilo, mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela, Mhe.Renatus Mulunga ameweka msisitizo kwenye kujipanga vyema na maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza katika mwaka mpya wa masomo 2025.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.