“Tunachotaka ni kuona wananchi wetu wanapata maji maana wasipopata maji uongozi wetu unakuwa hauna thamani yoyote tunawasaidiaje wananchi wetu?, Ilemela hakuna kijiji hoja ya msingi maji yawepo maeneo yote”
Ni Kauli iliyotolewa na Mhe. Hussein Magera Diwani wa Kata ya Ibungilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii akichangia hoja ya changamoto ya maji Wilayani Ilemela iliyoibuliwa kupitia maswali ya papo kwa hapo katika Baraza la Madiwani robo ya nne siku ya Tarehe 11 Agosti 2023.
Akichangia hoja hiyo Mhe Jonathan Mkumba diwani wa Kata ya Nyakato alisema kuwa mgao wa maji umegeuka kero zaidi hasa pale maji hayo yanapotoka usiku wa manane wakati watu wamelala na kuhoji maji yanapotoka usiku wa manane watachota saa ngapi?
Kwa upande wake Diwani kutoka Kata ya Buswelu Mhe Sarah Ng’hwani yeye alihoji juu ya ukosefu wa maji katika kata yake hali ya kuwa Wizara ilishatoa fedha kwa ajili ya utatuzi wa changamoto hiyo na kusisitiza kuwa anataka majibu sahihi ya kuwaeleza wananchi wake.
Katika Nyakati tofauti wakichangia hoja hiyo ya kero ya maji, Waheshimiwa Madiwani walisema kuwa MWAUWASA wamekuwa wakitoa ahadi ambazo hazitekelezeki hivyo kuwataka waje na majibu sahihi ya utatuzi wa kero hiyo ndani ya Wilaya ya Ilemela na kushauri iwapo MWAUWASA wameshindwa kutoa huduma hiyo ni vyema ikabinafsishwa ili wananchi waweze kutatuliwa kero hiyo.
“Ni wakati sasa wa MWAUWASA kuweka wazi tatizo ambalo linalopelekea changamoto hiyo ya maji kuwa kubwa Wilayani Ilemela na niwashauri mnapoongelea kuhusu uhaba wa maji ilemela muongelee kwa wilaya nzima na pia mje na majibu sahihi ili tatizo liweze kutatuliwa”amesema Mhe . Wilbard Kilenzi , diwani wa kata ya Ilemela.
Akijibu hoja hizo Mhandisi Stanley William, Meneja wa miundombinu MWAUWASA alifafanua juu ya kero hiyo ya maji na kukiri kuwa wamezidiwa kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji katika jiji la mwanza kuwa kubwa ambapo mpaka sasa lita za ujazo milioni 160 zinahitajika kwa siku na uzalishaji wa sasa ni milioni 90 kwa siku
“Upo upungufu wa maji kutokana na kuwa uzalishaji wa maji na mahitaji unatofautiana kwa kiasi kikubwa ndio maana tunategemea kukamilika kwa kituo cha Butimba kitakuja kupunguza adha ya maji kwani unataraji kuzalisha lita milioni 174, na ikiongezwa na kituo cha Kabangaja tatizo la maji litaisha kwani maji yatakuwa ya kutosha, tukiwa na maji ya kutosha wananchi wote watapata maji”, amesema Mhandisi Stanley
Kuhusu Kata ya Buswelu kukosa maji alifafanua kuwa hapo awali kulikuwa hakuna mabomba ya kutosha ya kuwafikia wananchi hivyo tenki la maji buswelu lilipokamilika maji mengi yalikuwa hayana pa kwenda kufuatia hali hiyo, walitawanya maji kuwasaidia wananchi ambao walivuta mbali kuwasogezea laini karibu ili wapate presha ya kutosha pamoja na kuwafikia wananchi ambao hawakuweza kuvuta maji.
Mhandisi Stanley alihitimisha kwa kusema kuwa kuboreka kwa huduma ya maji Ilemela na Mwanza kwa ujumla ni baada ya kukamilika kwa mradi wa maji Butimba ifikapo oktoba 2023
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.