Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Ilemela kupitia kikao maalum kilichoandaliwa kati yao na TARURA wamehimiza suala zima la ushirikishwaji katika mchakato mzima wa uboreshaji miundombinu ya barabara kupitia TARURA kuanzia zoezi la kutambua na kuainisha maeneo ya barabara kwa ajili ya matengenezo ya miundo mbinu ya barabara ya Ilemela.
Akifafanua umuhimu wa madiwani kushirikishwa katika kuainisha vipaumbele katika hatua za mwanzo za kuandaa bajeti za TARURA Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga alisema kuwa wao ndo wanajua chungu na tamu ndani ya kata zao kwani wanafahamu kona zote katika kata zao na kujua barabara ipi ni muhimu zaidi kulingana na shughuli zinazotendeka katika eneo husika.
Akichangia mjadala huo Diwani wa kata ya Shibula Mheshimiwa Swila dede Swila alisema kuwa vizuri TARURA wanapokuwa katika mchakato wa kuandaa bajeti zao kuwashikirisha ili waweze kutoa mapendekezo ya maeneo na barabara ambazo ni vipaumbele kutokana na uwepo wa muda mrefu katika kata zao na kuongeza kwa kusema kuwa yapo maeneo mengine wakati wa mvua hayapitiki kabisa.
Madiwani hao walipata fursa ya kuchangia na kutoa mapendekezo yao kuhusu maboresho mbalimbali ya barabara zilizopo kwenye maeneo yao lakini pia wameweza kuorodhesha barabara ambazo ni korofi, zenye kuhitaji matengenezo ya haraka na ambazo hazijaingizwa kwenye mpango wa mwaka huu fedha.
Mhandisi Sobe Makonyo ambae ni meneja wa Wakala wa serikali wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) Ilemela amesema kuwa kwa Manispaa ya Ilemela wametenga jumla ya shilingi bilioni 3,792,311,410 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya miundo mbinu ya barabara kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022.
Mhandisi Sobe aliendelea kufafanua katika kikao hicho maalum cha TARURA kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya mpango kazi wa utekelezaji wa miradi ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa madiwani wa manispaa ya Ilemela, na kusema kuwa chanzo cha fedha hizo ni fedha za matengenezo kutoka mfuko wa barabara(road fund) kiasi cha shilingi bilioni 1,294,311,410.53,fedha za majimbo kiasi cha shilingi milioni 500,000,000,fedha za maendeleo kiasi cha shilingi milioni 500,000,000 na fedha ya nyongeza kutoka bajeti ya TARURA shilingi bilioni 1,000,000,000.
“Tunatambua umuhimu wa barabara katika matumizi mbalimbali ya kijamii , kiuchumi na tija zake katika masuala ya kimaendeleo na ndicho kigezo kikubwa tunachokiangalia,ila waheshimiwa naomba tutambue kwamba tayari bajeti hii imeshapita katika vikao mbalimbali ngazi ya Wilaya hadi taifa na kwamba kuna baadhi ya maeneo kazi zimeshaanza na kwingine mikataba inaendelea kusainiwa”, amesema mhandisi Sobe.
Aliendelea kusema kuwa anafahamu kiu ya madiwani ya kutengenezewa barabara katika kata zao ila kulingana na bajeti ya mwaka huu wataigawa kidogokidogo na kwa maeneo yatakayobaki wataingiza katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Baadhi ya barabara ambazo zipo kwenye mpango wa matengenezo ni pamoja na barabara ya Sabasaba -Kiseke-Buswelu (9.63km), Mecco -Kaangae-Buswelu(2.81km),Karume-Kifuawazi(0.85km),baranara ya Breweries(2.5km) na barabara ya Tia yenye urefu wa km 0.08 ambapo kwa pamoja barabara hizo zimetengewa kiasi cha shilingi milioni 219.
“Tunatarajia kutengeneza zaidi ya barabara 20 zenye urefu km 94.74 kwa viwango tofauti vya lami,zege,mawe na marekebisho madogomadogo sambamba na ujenzi na utengenezaji wa madaraja na uchimbaji wa mitaro katika baadhi ya barabara.”amesema mhandisi Sobe.
Nae kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ndugu Shukrani Kyando amewashukuru wataalam wa TARURA kwa ushirikiano wao wanaoendelea kuuonyesha kwa manispaa ya Ilemela na kuahidi kutoa ushirikiano chanya katika kufanikisha maboresho ya miundo mbinu ya barabara inayochochea maendeleo kwa kasi ndani ya Wilaya ya Ilemela.
Mtandao wa barabara ndani ya manispaa ya Ilemela unaosimamiwa na TARURA una urefu wa km 875.85 ambapo barabara za lami ni km 35.26, zege km 1.52, mawe km 2.17, changarawe km 72.68 na udongo ni km 764.22 sawa na asilimia 87 ya mtandao mzima.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.