Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe Hassan Masala amekabidhi jumla ya madawati 710 kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ambayo yatatolewa kwa shule 33 za Msingi katika Manispaa hii ikiwa ni matokeo ya harambee iliyoratibiwa nae siku ya tarehe 31 Mei 2022.
Mhe, Masala akizungumza wakati wa zoezi hili amesema kuwa hii ni awamu ya pili ya utoaji wa madawati haya ambapo awamu ya kwanza yalikabidhiwa madawati 431 kwa shule 21 na awamu hii ya pili yamekabidhiwa madawati 710 lengo kubwa ikiwa ni kupunguza changamoto za kujifunza na kujifunzia, kwa wanafunzi wa shule za msingi ilemela.
“Hatujisikii vizuri kama wazazi na viongozi tuliopewa dhamana ya kumsaidia Mhe Rais kuona watoto ya jamii ya watu tunayoiongoza wanakosa mazingira ya bora ya kupata elimu na ndio maana tuliweka mkakati wa pamoja ambapo tuliwashirikisha wadau”, Mhe Masala amesema.
Aidha amesisitiza juu ya suala la ugawaji wa madawati haya kuzingatia usawa na kuwa isitokee upendeleo wa aina yoyote ile na madawati haya yatolewe kutokana na mahitaji ya maeneo husika kwa kuzingatia shule zenye uhaba wa madawati.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary mbali na kuwashukuru wadau mbalimbali waliochangia upatikanaji wa madawati haya, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa jitihada zake za kusaidia watoto wa Ilemela waweze kukaa na kupata maeneo ya kujifunzia huku akimuomba kuendelea kutumia wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuisimamia Wilaya ili kuweza kuileta maendeleo Wilaya ya Ilemela.
“Nikushukuru Mkuu wa Wilaya kwa jitihada hizi zakusaidia watoto wa Ilemela waweze kukaa na kupata maeneo ya kujifunzia, pia nikuombe uendelee kutumia wadau na kutusimamia ili tuweze kutekeleza wajibu wetu katika kuiletea maendeleo Wilaya yetu”, Mhandisi Modest amesema
Ndugu Yusuph Bujiku, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela, amepongeza jitihada hizi huku akiwataka wananchi kuwa mabalozi wazuri wa shughuli za serikali zinazofanyika, kwani haya yote yanayofanyika ni maono ya Mhe Rais yeye anatoa dira na anapotoa dira viongozi hutekeleza hivyo niwaombe wananchi tumpe ushirikiano kwa sababu kazi tunaziona na hivyo tuwe mabalozi wazuri wa kuwaeleza watu wengine kuwa serikali yetu inayo mambo inaendelea kufanya, amesisitiza
Akihitimisha zoezi hili la utoaji wa madawati Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela ametoa rai kwa watu wote kuhakikisha kuwa wanayatunza madawati hayo kwani ni lazima kuthamini na kutambua kuwa hizi ni fedha zilitolewa na wadau wa maendeleo. Huku akisisitiza suala la ushirikiano kwani haya yote yamewezekana kwa ajili ya ushirikiano uliopo chini ya kauli mbiu ya Ilemela isemayo, “Ilemela ni yetu Tushirikiane kuijenga”.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.