Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi.Ummy Wayayu ametembelea kambi ya madaktari bingwa wa Dkt.Samia hospitali ya Wilaya ya Ilemela iliyopo mtaa wa Isanzu kata ya Sangabuye kuona namna huduma za kibingwa zinavyotolewa kwa ubora hali iliyopelekea ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma za Afya na ushauri wa kitaalamu.
Akitoa taarifa ya zoezi linavyoendelea Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya Ilemela Dr.Mateso Mayunga amesema huduma za kibingwa za magonjwa ya watoto, wanawake,upasuaji,magonjwa ya ndani na huduma za usingizi na ganzi salama zinaendelea kutolewa.
“ Mpaka sasa jumla ya wagonjwa 140 wameshahudumiwa ikiwa ni zaidi ya asilimia 100 ya wagonjwa wanaohudumiwa kwa siku katika hospitali yetu sambamba na makusanyo ya shilingi milioni 1.3 kwa siku nne za uwepo wa madaktari bingwa .”
Bi.Ummy amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu mkubwa wa wananchi wa kawaida kusogezewa huduma hizo za kibingwa.
Aidha madaktari hao wamewawezesha kwa vitendo madaktari wenyeji namna bora zaidi za kutoa huduma za afya kwa wananchi kwa kutumia vifaa bora na vya kisasa vilivyopo katika hospitali hiyo na kutoa maoni na mapendekezo ya aina ya vifaa na huduma za kuongezwa zaidi katika kuleta ufanisi ki utendaji.
“Tumefanikiwa kufanya oparesheni mbili kwa mafanikio makubwa,sisiti kusema kuwa hospitali hii inaweza kufanya makubwa zaidi ya haya kikubwa ni kubuni mbinu za namna ya kuwavutia wateja kwa kuboresha utoaji wa huduma zetu.” Dkt.Peter Kyamba bingwa wa upasuaji.
Nae Dkt.Irene Makundi bingwa wa magonjwa ya ndani amewataka wananchi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kufuatilia kwa karibu afya zao kwani inaonyesha watu wengi ni wagonjwa na hawajijui.
“ Kwa siku hizi nne nimekuwepo hapa wagonjwa wengi wana shida ya presha,wanatembea na presha ipo juu sana wengine ipo chini na wanaendelea na shughuli zao hali ambayo ni hatari kiafya.”Dkt.Irene Makundi bingwa wa magonjwa ya ndani.
Madaktari hao wamepongeza mazingira ya usafi yaliyopo hospitalini hapo huku wakipongeza timu nzima ya watumishi kwa namna ambavyo wanafanya kazi kwa ushirikiano na kusisitiza uongozi wa Ilemela kuweka mazingira rafiki ya wananchi kufika kwa urahisi kupata kuhuduma za afya.
Mkurugenzi Ummy amepokea maoni na mapendekezo ya madaktari hao huku akiahidi kufanya maboresho ya miundo mbinu na huduma kwa wateja, kuongeza vifaa na dawa huku akithibitisha kuendelea kupokea fedha nyingi kutoka serikali kuu kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ndani ya Manispaa yake.
Magdalena Shija ni mkazi wa mtaa wa Sangabuye,yeye ni mmoja wa wagonjwa waliopatiwa huduma ya afya na Dkt.Makundi anapongeza sana huduma nzuri aliyoipata na kuiomba serikali iendelee na utaratibu huo wa kusambaza madaktari maeneo ya nje ya miji kwani ni fursa kwa wananchi wa hali za chini kupata huduma.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.