Wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la machinga wametakiwa kutorudi katika maeneo ya awali ambayo si salama kwaajili ya kufanya biashara zao.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala wakati akizungumza na wenyeviti wa Serikali za mitaa, watendaji wa kata, watendaji wa mitaa, viongozi wa masoko, wataalam wa biashara na masoko wa wilaya ya Ilemela na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo ambapo amesikiliza kero na changamoto zinazokabili wafanya biashara hao kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi huku akiwataka kutorejea maeneo ya awali waliyokuwa wakifanyia biashara ambayo si salama kwao na biashara zao badala yake kuwaasa kubaki katika maeneo waliotengewa na Serikali kwaajili ya kuendelea na biashara zao kwani Serikali imetumia gharama kubwa kuwawekea miundombinu ikiwemo maji, umeme, barabara na huduma nyengine za msingi ikiwemo taa ili waweze kufanya biashara zao kwa amani na utulivu.
‘.. Hakuna Serikali inayotaka watu wake wateseke, Tumejitahidi kuwaboreshea miundombinu ya masoko kama mlivyotaka, Na tutaendelea kufanya hivyo kwa kadri ya mahitaji ya wakati, Niwaombe wafanyabiashara wasirudi maeneo hatarishi, Watu wote wafanye biashara katika maeneo tuliokubaliana ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala amewapongeza wafanya biashara wa wilaya hiyo kwa ushirikiano walioutoa wakati wa zoezi la kupanga wafanya biashara wadogo kwani lilienda vizuri kwa amani na utulivu tofauti na maeneo mengine huku akiwataka kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Rais Samia Suluhu Hasan katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
Nae katibu tawala wa wilaya hiyo, Ndugu Said Kitinga amefafanua kuwa Serikali haitamvumilia mfanyabiashara yeyote atakaekaidi maagizo yake huku akiwaasa wanasiasa kutoingilia mchakato wa kuwapanga wafanyabiashara katika maeneo rasmi na kwamba hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria hivyo ni muhimu kutii sheria bila shuruti.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Joseph Apolinary amesema kuwa manispaa yake ilishatenga bajeti ya kuhudumia masoko ya wilaya hiyo hivyo kero na changamoto zote zitakuwa zikipatiwa ufumbuzi kwa kadri ya zitakavyojitokeza pamoja na kuwaagiza wataalam wa manispaa hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa na masoko kubainisha mahitaji ya masoko ili yaweze kushughulikiwa.
Akihitimisha kikao hicho katibu msaidizi wa soko la Nyasaka senta Bwana Laurent Alphonce mbali na kuishukuru Serikali kwa kuboresha masoko yake ameiomba kuwarejesha ndani ya soko wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao nje ya soko kwa kuwa eneo hilo si salama sanjari na kupunguza vibanda vya soko hilo kwani idadi ya wafanyabiashara ni ndogo ukilinganisha na vibanda vilivyopo jambo linalokwamisha shughuli za ulinzi wa eneo hilo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.