Kuelekea maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza yanayoadhimishwa kila mwaka halmashauri ya manispaa ya Ilemela kupitia idara ya afya kitengo cha lishe imeanza kutoa elimu ya lishe bora na namna ya kuepuka magonjwa hayo kwa watumishi katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ni katibu tawala wa Wilaya ya Ilemela Adv.Mariam Msengi amesema lishe ni moja kati ya vipaumbele muhimu katika serikali ya awamu ya sita kwa kutambua kuwa lishe bora ni chachu ya kuwa na wananchi waelewa na wenye manufaa makubwa kwa taifa lao.
“Tumeshuhudia mikataba mingi ya mambo ya lishe ikisainiwa katika ngazi za kitaifa ,hiyo yote inaonyesha kuwa Rais wetu anahitaji taifa lisonge mbele likiwa na wananchi wenye lishe bora sambamba na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo mbalimbali yenye tija.”
Akitoa elimu hiyo ya lishe bora Mratibu wa lishe wa Manispaa ya Ilemela Bi.Pili Khassim amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa mengi kwa sababu ya mitindo ya maisha tunayoishi na kuongeza kuwa ipo haja ya kubadili mitindo ya maisha yetu ya sasa ili kupambana na magonjwa yasiyoambukizwa kama vile magonjwa ya moyo na figo.
“Familia siku hizi zinaendeshwa na watoto badala ya wazazi /walezi kuziendesha.Watoto wakitaka chips,burger au pizza wanapewa wengine hata kila siku tunahisi tunaonyesha upendo kwa watoto bila kujua kuwa tunawapa lishe hatarishi kwa miili yao kutokana baadhi ya vyakula hivyo kuwa na mafuta mengi yasiyofaa.”
Bi. Pili amesisitiza watu kuzingatia lishe bora inayofaa kwa kula makundi matano ya vyakula ambayo ni vyakula vya nafaka,jamii ya kunde,mbogamboga,matunda,mafuta na sukari bila kusahau maji kwa kuzingatia mchanganyiko unaofaa.
Nae Afisa lishe wa Manispaa Bi.Joyce Albert ametoa elimu juu ya mitindo bora ya maisha kwa kuzingatia lishe bora yenye uwiano sahihi sambamba na kufanya mazoezi mepesi kama kutembea hali inayoweza kupunguza uwezekano wa kupata baadhi ya magonjwa kama kisukari,baadhi ya aina za saratani na shinikizo la damu.
“Ili tupate kizazi bora ni lazima kuzingatia lishe bora hasa kwa watoto chini ya miaka miwili kwa kuzingatia ulaji unaofaa.” Amesema Bi.Joyce.
Neema Kipeja ni mmoja wa watumishi waliopata elimu hiyo ya lishe bora yeye anashukuru uongozi wa idara ya afya kwa kuona umuhimu wa kuanzia ndani katika kutoa mafunzo hayo.
" Somo la maandalizi ya chakula cha mtoto kwa kuchanganya nafaka chache au kutochanganya kabisa limekuwa zuri kwa kuzingatia kuwa wengine tuna watoto wadogo ambao bado hawajaweza kula wenyewe,kuzingatia usafi na ubora wa nafaka au vyakula kabla ya kuandaliwa ni muhimu kuepuka kula vyakula ambavyo vimeharibika.”
Sambamba na mafunzo hayo vipimo mbalimbali vya kiafya kama vile kupima uzito,urefu,hali ya lishe,kipimo cha presha na ushauri wa kiafya vilitolewa bure pamoja na zoezi la uchangiaji damu.
Maadhimisho hayo ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza kwa mwaka huu 2023 yamebebwa na kauli mbiu isemayo "usijisahau jali afya yako".
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.