Kamati ya bunge ya kudumu ya hesabu za serikali za Mitaa (LAAC) ambayo imeongozwa na Makamu Mwenyekiti, Mhe Selemani Zedi (Mb), imeridhishwa na namna Manispaa ya Ilemela imekuwa ikisimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ambapo wamekagua miradi miwili ambayo ni stendi mpya ya mabasi na maegesho ya malori pamoja na ujenzi wa Jengo la utawala.
Wakikagua mradi wa ujenzi wa jengo la utawala wamesema kuwa wamefarijika kukuta kuwa ujenzi huu umefikia asilimia 65, kwani mwaka 2019 walipokuja na kamati hii walikuta mradi umetelekezwa na mkandarasi (TBA) ambapo waliishauri Manispaa kuvunja mkataba na Halmashauri ikazingatia ushauri huu na sasa mradi upo hatua nzuri
“Niseme tu kwamba tofauti na kipindi kile tumekuja 2019 sasa hivi tunaona kwamba usimamizi wa shughuli za kimaendeleo, fedha za umma zinazoletwa kutekeleza miradi mbalimbali mkoani Mwanza umeboreka na kuimarika, hivyo kamati tumeridhishwa na maendeleo ya ujenzi huu ”, amesema Mhe. Selemani Zedi (Mb)
Waliongeza kusema kuwa wanayo imani kuwa kufikia mwezi wa sita jengo litakuwa limekamilika kwa asilimia 100 kama ambavyo taarifa imesomwa ili watumishi wapate sehemu nzuri ya kufanyia kazi na wananchi wapate huduma bora.
Kamati hiyo ilipata fursa ya kukagua stendi ya mabasi na maegesho ya malori iliyopo Nyamhongolo na kusema kuwa wameshuhudia ubora wa hali ya juu katika majengo yote waliyotembelea na kuwa wameridhishwa na namna Mkoa, Wilaya na Halmashauri inamsaidia Mhe Rais katika usimamizi na utekelezaji wa miradi.
“Huu mradi ni mkubwa sana na Shilingi Bilioni 26 ni fedha nyingi sana na mmezisimamia vizuri sana ni jambo la faraja kwamba thamani ya mradi mwanzoni ilikuwa ni shilingi Bilioni 28 lakini kwa usimamizi mzuri mmeweza kutekeleza mradi huu kwa shilingi bilioni 26 hivyo mmeokoa shilingi bilioni 2 kamati inawapongeza sana” Alisema Makamu Mhe Selemani Zedi(Mb)
Pamoja na kuipongeza Ilemela kwa utekelezaji mzuri wa miradi, wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge walishauri kuwa itafutwe namna bora ya uendeshaji wa mradi wa stendi ya Mabasi na Maegesho ya malori kwa kuangalia wawekezaji wenye uwezo wa kuendesha biashara eneo hili, pamoja na hilo kuepusha kuwa na biashara ndani ya biashara na kuhakikisha kuwa stendi hii inaendeshwa kidigitali ili mradi uwe endelevu na uweze kuleta tija kwani lengo kubwa la uanzishaji wa miradi hii ya kimkakati ni kuondoa utegemezi wa Halmashauri kwa serikali kuu.
Aidha zilitolewa pongezi kwa chuo kikuu cha Dar es Salam kitivo cha uhandisi kwa kubuni mchoro wa jengo hili la stendi na maegesho pamoja na kusimamia hadi kukamilika, na kusema kuwa wanajivunia kwamba jengo hili limebuniwa na kusimamia na watanzania
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, aliishukuru kamati hiyo ya Bunge kwa kufika Mkoani Mwanza na kuahidi kupokea na kuyatekeleza maelekezo, maoni na ushauri wote utakaotolewa na kamati hii huku akisisitiza kuwa Mwanza haitakuwa sababu ya kukwamisha maelekezo ya serikali
“Mwanza haitakuwa sababu ya kukwamisha maelekezo ya serikali haitakuwa sababu ya kukwamisha ndoto na dira za mhe Rais, Mwanza haitakuwa kikwazo kutekeleza maelekezo na maagizo ya bunge la Jamhuri, Mwanza tumekubali kuleta mapinduzi na mageuzi kwa kutumia akili, utashi nguvu na maarifa hatutakubali Mwanza kuwa kichaka cha uharibifu, uovu na vurugu zaidi katika upande wa usimamizi wa miradi ya maendeleo”,Alisema Mhe Robert Gabriel
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.