Ujenzi wa barabara za Buswelu - Nyamadoke -Nyamhongolo (Km 9.5) na Barabara ya Buswelu - Busenga -Cocacola (Km 3.3) unatarajiwa kuwa ni wenye manufaa makubwa kwa wananchi wa Manispaa ya Ilemela pamoja na maeneo ya jirani kwa kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi na kuvutia uwekezaji na kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali Wilaya ya Ilemela .
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Sobe Makonyo (Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilemela) alipokuwa akisoma taarifa ya mradi mbele ya kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Ndg Ismail Ali Ussi siku ya Jumanne ya tarehe 26 Agosti 2025
Aidha Mhandisi Sobe akisoma taarifa hiyo alifafanua kuwa lengo la mradi huu ambao hadi sasa umefikia asilimia 88 ya ukamilishajini kutatua kero ya ubovu wa barabara na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi ambapo hadi kukamilika kwake ujenzi huu utagharimu shilingi 23,490,242,253.00
Akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara hii, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Ismail Ussi aliwataka wananchi wa Ilemela kuwa wavumilivu kwani hatua ya ujenzi wa barabara hii ilipofikia matunda yake yataonekana muda si mrefu huku akiwapongeza wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa usimamizi na ujenzi wa barabara za ndani zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
“Kama kulikuwa kuna mwananchi ana dhana ya kuwa barabara hii itaendelea kuwa ni hadithi katika maeneo yetu kwa kweli dhana hiyo itabaki kuwa ni hadithi katika kichwa chake, ni kwa sababu ya kiwango kikubwa cha uwekezaji katika barabara hii, mimi binafsi mpaka nimefika hapa nilikuwa najionea utofauti wa hali ya juu, ndugu wananchi endeleeni kuwa wavumilivu kwani hatua ya ujenzi barabara hii ilipofikia muda si mrefu mtayaona matunda yake”. Alisema Ndg Ussi
Sambamba na uwekaji wa jiwe la msingi katika barabara hiyo, Mwenge wa Uhuru 2025 ulizindua mtambo wenye thamani ya shilingi Bil. 1.156 utakaotumika kuboresha miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Ilemela.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.