"Dhamana mliyopewa ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na wabunge wa Jamhuri ya Muungano na madiwani kwa Tanzania Bara ni kubwa,nyeti na muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu, hivyo mnategemewa kuzingatia utendaji wenu na muwajibike ipasavyo hadi tutakapokamilisha jukumu hili la uchaguzi mkuu"
Kauli hiyo imetolewa na Ndugu Herbert Bilia ambae ni msimamizi wa uchaguzi jimbo la Ilemela leo tarehe 04 Agosti 2025 wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Aidha amewataka kuzingatia na kufuata hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na kisheria sambamba na kusoma katiba, sheria, kanuni taratibu miongozo na kufuata maelekezo yote yatakayokuwa yakitolewa na tume huru ya taifa ya uchaguzi.
Pamoja na hayo Ndugu Bilia amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuisoma miongozo yote, kushirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili, kuvitambua mapema vituo vya kupigia kura ili kubaini mahitaji maalum kama yapo, kuhakiki vifaa vya uchaguzi, kutoa taarifa mapema kwa vyama vya siasa wakati wa kuwaapisha mawakala wao, sambamba na kuzingatia muda wa kufungua kituo cha kupigia kura.
Mafunzo hayo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata 38 kutoka kata 19 ambayo yataendeshwa kwa siku tatu kuanzia tarehe 04 hadi 06 Agosti yametanguliwa na washiriki wa mafunzo hayo kuapa kiapo cha kutunza siri pamoja na tamko la kujitoa katika vyama vya siasa zoezi lililo ongozwa na Hakimu mfawidhi wa mkoa wa Mwanza Mhe Bonaventure Michael Lema ambae amewasisitiza kusimamia viapo vyao.
"KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KUPIGA KURA"
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.