Kuelekea kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika Disemba 09 wananchi wa Ilemela wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya usafi katika mazingira yanayowazunguka.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela ndugu Said Kitinga wakati akizungumza na wananchi na wafanyabiashara wa soko la Kiloleli lililopo kata ya Ibungilo mara baada ya shughuli ya usafi iliyofanyika sokoni hapo.
“Amani na umoja ni nguzo ya maendeleo yetu” ndio kauli mbiu ya maadhimisho haya,hivyo tunao wajibu wa kuendelea kuwa na mazoea ya kufanya usafi katika maeneo yetu yote ya makazi na biashara, suala la usafi hulinda afya zetu na kutunza mazingira kwa ujumla.”Amesema Kitinga
Ndugu Kitinga ameongeza kusema kuwa Tanzania imekuwa ikipiga hatua katika sekta zote kimaendeleo akitolea mfano kwa upande wa sekta ya elimu kuwa yapo mabadiliko mengi yanayoendelea katika Manispaa ya Ilemela ambapo miundombinu mbalimbali ya shule ikiwemo madarasa inaendelea kujengwa na kusema kuwa Ilemela ilipokea kiasi cha Shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 110 kwa shule za sekondari na kuongeza kuwa fedha ni nyingi zimetolewa na zinaendelea kutolewa na kuwahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono jihudi za serikali katika kuleta maendeleo
Nae mwenyekiti wa soko la Kiloleli Kalala Egata ameushukuru uongozi wa manispaa ya Ilemela kwa kuchagua soko hilo kujumuika kufanya usafi kama eneo la mfano kwa maeneo mengine ndani ya Manispaa hiyo huku akiwataka wafanyabiashara sokoni hapo kuyaishi maelekezo ya usafi wa mazingira kila siku.
“Masoko yapo mengi ila leo tumechaguliwa sisi Kiloleli katika shughuli hii kuhamasisha wengine naomba tuyaishi maelekezo na maagizo ya kufanya usafi wa mazingira bila shuruti nyakati zote mahali popote.”Amesema Egata
Kila mwaka ifikapo tarehe 09 Disemba Tanzania huadhimisha miaka kadhaa toka kupata uhuru wake na kwa mwaka 2022 sherehe hizi zimetanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira ambapo uongozi wa Wilaya ya Ilemela wamejumuika na wafanyabiashara katika soko la kilole kufanya usafi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.