“Nichukue fursa hii kuonyesha furaha yangu ya dhati nikiwa kama mwanamichezo kwa kukamilika kwa ujenzi wa kituo hiki cha michezo, kwani huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala wa kuendeleza michezo Tanzania” ,Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongela alipokuwa akihutubia kadamnasi iliyofika kushuhudia uzinduzi wa kituo hicho.
Akizindua kituo hiki Mhe. Mongela, ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kuhakikisha kuwa, inaweka nguvu zaidi katika kulipendezesha eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa inaweka uzio kwani ukitaka kubebwa ni lazima ubebeke, Alisistiza
Aliendelea kusisitiza kuwa wana michezo wote kuunga mkono wito wa taasisi ya Sport Charity kuwa jamii inatakiwa ijitokeze kufanya mazoezi katika viwanja hivi ili wafadhili wapate moyo wa kuendelea kufadhili.
Pamoja na hayo ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji ili kuweza kukamilisha ujenzi wa eneo hilo na kuahidi kuendelea kutafuta wafadhili mbalimbali kwa ajili ya kukiendeleza kiwanja hiki.
Kituo hiki ambacho kimefika takribani asilimia 90 za ukamilishaji kimegharimu kiasi cha shilingi za kitanzania Milioni mia moja na sitini kinajumuisha viwanja vinne vya michezo ambavyo ni kiwanja cha mpira wa miguu, mpira wa wavu, mpira wa pete pamoja na mpira wa kikapu.
“Akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hiki kwa mgeni rasmi, Ndugu Isack Mwanahapa ambae ni katibu wa taasisi ya “Sports Charity”, ametoa shukurani kwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwa kukubali kutoa eneo hilo ili liweze kutumika kwa ajili ya michezo.
Pia alimshukuru Mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe.Dkt.Angeline Mabula kwa jitihada zake za kufuatilia kwa karibu na kutoa msaada mara zote unapohitajika pamoja na kutoa hamasa ya ujenzi kwa kuchangia tofali takribani 1000.
Pamoja na shukurani hizo alizozitoa, aliomba kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali kubwa hasa ikiwemo eneo la kituo hicho cha michezo kutumika na wafanyabishara hasa siku yam nada jambo ambalo linaweza kudhoofisha uboreshaji wa kiwanja hicho pamoja na kupelekea nyasi na miti kutokustawi na pia litaharibu ubora wa uwanja huo.
Nae Naibu Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe.Wilbard Kilenzi ambae pia ni diwani wa kata ya Ilemela ambapo kituo hicho kimejengwa akitoa shukurani zake amewaomba wafadhili kufikiria suala la kuleta walimu wenye taaluma ya michezo, kwani vipaji vipo vingi ila inashindikana kuvikuza kutokana na ukosefu wa wataalam wa kutosha wa michezo.
Mhe.Dkt Angeline Mabula, Mbunge wa Ilemela amewashukuru wafadhili hao kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho na huku akisisitiza uwepo wa timu nyingi na za kutosha ili kuweza kufanya mazoezi kwani michezo ni afya na pia uwepo wa kituo hicho cha michezo itapunguza vijana kukaa vijiweni italeta ajira huku akiwataka wana Ilemela kujitokeza kwa wingi kutumia viwanja hivi.
Bi Estelle Brulhart, mwakilishi wa wafadhili kutoka ujerumani, ufaransa,uswizi wakiwemo wanafunzi na watu binafsi, amewashukuru wote walioshiriki katika ujenzi wa kituo hiki na kusema kuwa anaendelea kuwatia moyo wachezaji kuendelea kufanya mazoezi kwani michezo ni afya.
Akihitimisha , Afisa Tarafa ya Ilemela Ndugu Mzava kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuendelea kuielea Ilemela na pia kwa msaada aliotoa wa mifuko ya saruji huku akitoa maelekezo kwa wafanyabiashara wanaotumia eneo hilo siku ya mnada kuhamia eneo lingine ambalo wataonyeshwa ili kupisha eneo la viwanja hivyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa viwanja hivyo vinatunzwa na kulindwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
Hiki ni kituo cha pili kujengwa na taasisi ya Sports Charity Mwanza kwa kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa michezo kutoka nchi za Ujerumani,Ufaransa, na Uswisi Kukamilika kwa uwanja huu kutasaidia kuibua vipaji mbalimbali katika sekta ya michezo, kutengeneza ajira kwa vijana na jamii kwa ujumla, pia kupambana na magonjwa yasiyoambukizwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.