Kaya zaidi ya 374 zinatarajiwa kunufaika na mradi wa watoto waliopoteza malezi na ambao wapo kwenye hatari za kimalezi kwa manispaa ya Ilemela chini ya ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la SOS Childrens Villages Mwanza
Akizungumza na wataalam wa manispaa ya Ilemela katika ukumbi wa jengo jipya la utawala wakati wa utambulisho wa mradi huo Kaimu meneja miradi kutoka shirika la SOS Children jijini Mwanza Bi Elizabeth Swai amefafanua kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuhudumia watoto walio katika hatari ya kupoteza malezi ili kwenda sambamba na dira ya serikali katika kupunguza kama si kuondoa kabisa watoto kulelewa katika makao badala yake kuifanya jamii itimize wajibu wake katika malezi
‘.. Tunataka tukamjengee uwezo mzazi au mlezi ili aweze kutimiza wajibu wake katika malezi, Awe na uwezo wa kielimu kutambua fursa na changamoto katika malezi, Tukasaidie familia ambazo watoto wamekata tamaa, Familia tunazodhani tusipozisaidia mtoto ataona bora atoroke nyumbani, bora akaombeombe ..’ Alisema
Aidha Bi Swai ameushukuru uongozi wa manispaa ya Ilemela na idara ya maendeleo ya jamii kwa namna wanavyoshirikiana na taasisi yake katika kusaidia jamii na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kupitia utekelezaji wa afua tofauti tofauti
Kwa upande wake afisa mradi Bi Kokutona Kayungi ameongeza kuwa mradi huo utagusa kata za Kayenze, Sangabuye, Bugogwa, Shibula na Nyamhongolo ambapo wenyeviti wa mitaa, wasaidizi wa mashauri ya ustawi wa jamii na kamati za kubaini familia zinazostahili kuhudumiwa na mradi watahusishwa
Sarah Nthangu ni mratibu wa wa mpango huo ambae pia ni afisa maendeleo wa manispaa ya Ilemela ameshukuru kwa utekelezwaji wa mradi huo kwa manispaa ya Ilemela huku akiwaasa wataalam wenzake kuunga mkono mradi huo na kutoa ushirikiano ili utekelezeke kwa ufanisi na urahisi ili manufaa yaliyokusudiwa yapatikane
Uzinduzi wa mradi huo umehudhuriwa na watendaji wa kata, mitaa, maafisa ustawi, elimu, kilimo kwa ngazi ya kata na manispaa kutoka maeneo yatakayonufaika na mradi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.