Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imehawilisha jumla ya shilingi Milioni 143,704,00.00 kwa kaya 3912 kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF).
Akizungumza katika zoezi la uhawilishaji wa fedha hizo mratibu wa TASAF Manispaa ya Ilemela ndugu Frank Ngitaoh alisema kuwa hii ni awamu ya tatu tangu kuanza kwa mpango huo ikiwa na mzunguko wa kumi na sita uliojumuisha wanufaika wa mitaa yote ya kata kumi na nane za Kayenze, Sangabuye, Bugogwa, Shibula, Buswelu, Kiseke, Kirumba, Nyamhongolo, Nyakato, Nyasaka, Kawekamo, Pasiansi, Mecco, Buzuruga, Ilemela, Kitangiri na Nyamanoro zilizopo kwenye mpango ikiachwa kata moja ya Kahama ambayo haipo kwenye mpango huo. '.. Tumezifikia kaya 3912 zinazonufaika na mpango huu wa kunusuru kaya masikini katika mzunguko huu wa kumi na sita ambapo zaidi ya milioni mia moja na arobaini na tatu tutazihawilisha kwa walengwa kusudiwa ..' Alisema
Kwa upande wake afisa ufuatiliaji wa mpango huo wa kunusuru kaya masikini (TASAF) kwa mkoa wa Mwanza Ndugu Kagwe Samson Kagwe amewataka wananchi wanaonufaika na mpango huo kuhakikisha wanazitumia vizuri fedha hizo kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji itakayowakwamua kutoka katika umasikini huku akiwakumbusha kuwa serikali itawachukulia hatua watu wasio waadilifu na wale wanaokwamisha zoezi hilo pamoja na walengwa watakaotumia vibaya fedha hizo.
Nae Mwenyekiti wa mtaa wa Bugogwa ndugu Kongwe Aloyce Kongwe mbali na kuishukuru Serikali kwa kuendelea na mpango huo uliosaidia wananchi wake kuweza kumudu gharama za maisha ikiwemo kupeleka watoto shule, kuanzisha miradi midogo midogo ya bustani za mboga mboga na biashara ameiomba kuona namna bora itakayo wafanya watu wenye sifa ambao walipuuza kujiunga na mpango wa kunusuru kaya masikini wakati wa zoezi la kuhakiki wanufaika ili waweze kurudishwa kwenye mpango na kunufaika
Zoezi la uhawilishwaji wa fedha za mpango wa kunusuru kaya masikini lilihusisha pia utembeleaji wa kaya za mfano kuona shughuli za uzalishaji zinazofanywa na baadhi ya wanufaika wa mpango huo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.