Jumla ya kaya elfu mbili kati ya kaya elfu tano mia tatu arobaini na tisa zimefuzu na kuondolewa katika mpango wa kunusuru kaya masikini kwa wilaya ya Ilemela
Hayo yamebainishwa na mratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF Ndugu Leonard Robert ambapo amesema kuwa mwaka 2023 mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF ulitoa taarifa na kufanya zoezi la tathimini kwa walengwa ili kubaini kaya zilizoimarika kiuchumi na kukidhi vigezo vya kuondolewa kwenye mpango ambapo kwa wilaya ya Ilemela jumla ya kaya 3,349 zitaendelea kupokea malipo kutoka kwenye mpango huku akizitaka kaya imarika kuendelea kukutana katika vikundi na kupanga mipango na mikakati ya kujiendeleza kiuchumi
‘.. Kuondolewa katika mpango haimaanishi kwamba vile vikundi vyetu vya TASAF vimekufa, kaya zilizoimarika zinaweza kuendelea kukutana na zikatumia vikundi hivyo kupanga mipango ya kujiendeleza kiuchumi hata kunufaika na mikopo ya halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ..’ Alisema
Aidha Ndugu Leonard akaongeza kuwa zoezi la kubaini kaya zilizoimarika kiuchumi ni endelevu na kaya zitakuwa zikiondolewa kwa kadri ya zinavyofuzu katika mpango
Mkama Costantine Sururu ni mwezeshaji wa TASAF manispaa ya Ilemela katika kata ya Buzuruga ameshauri kaya zilizobaki na kuendelea na kunufaika na mpango kutumia fedha wanazopewa kwaajili ya shughuli za kiuchumi kwaajili ya kujiongezea kipato kwa kuwa ipo siku nao watatoka katika mpango sanjari na wale waliotoka kutumia fursa ya vikundi kukopa katika taasisi za fedha na halmashauri kama njia ya kujiimarisha kiuchumi
Nae mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa ustawi kata ya Buzuruga Ndugu Bahati Richard Kabadi mbali na kumshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa mpango huo wa kupunguza umasikini, akazipongeza kaya zilizotoka katika mpango wa kunusuru kaya masikini kwani walitumia vizuri fedha walizopata kwaajili ya shughuli za uzalishaji mali na kujiimarisha kiuchumi huku akisisitiza kaya zilizosalia kuiga mfano huo
Kwa upande wake Bi Pili Mtatiro Masigiti ambae ni miongoni mwa wana kaya zilizofuzu mpango kutoka mtaa wa Nyambiti ametaja faida alizozipata kutokana na TASAF ikiwemo kusomesha watoto na wajukuu zake, kukarabati nyumba yake, kuwa na uhakika wa chakula cha kila siku na kupata mtaji wa biashara tofauti na hali ya kiuchumi aliyokuwa nayo kabla ya kuwepo katika mpango
Manispaa ya Ilemela katika malipo ya dirisha la mwezi machi-aprili inatarajia kufanya malipo ya jumla ya kiasi cha Tshs 235,176,000 (Shilingi Milioni 235.17) kwa njia ya fedha taslimu, njia ya mtandao wa simu na benki kwa kaya 5349 zinazonufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini ikiwa ni pamoja na kaya zilizofuzu mpango ambapo haya yatakuwa malipo yao ya mwisho kabla ya kuondolewa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.