KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AIPONGEZA ILEMELA
Katibu Mkuu wa Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Mhe Dkt Mpoki Ulisubisya ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa ujenzi nafuu wa majengo ya Kituo cha Afya Karume ukihusisha mafundi wazawa ikiwa ni utekelezaji wa lengo la Serikali la kuhakikisha inaboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Hayo ameyasema wakati wa ziara yake aliyoifanya katika kituo hicho cha Afya mara baada ya kukagua majengo ya kutolea huduma za mama na mtoto likiwemo jengo la kuhifadhia maiti, jengo la upasuaji, jengo la maabara na nyumba ya watumishi
‘.. Niwapongeze kwa ujenzi bora na wenye gharama nafuu mliotumia mafundi wenu wa ndani na kama mnavyojua Mheshimiwa Rais John Magufuli ameweka juhudi kubwa sana katika kuhakikisha Serikali inaboresha huduma za afya, na hili limemtofautisha yeye binafsi kama mfanya kazi kwa bidii sasa ni kwa nini na sisi kila mmoja wetu asiwe kama yeye?, …’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mpoki amesisitiza juu ya kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya malaria huku akiitaka Ilemela kuwa manispaa ya mfano kati ya manispaa zote zilizo kando ya Ziwa Viktoria kwa kuwa na mafanikio makubwa katika mapambano ya udhibiti wa ugonjwa wa kipindupindu.
Kwa upande wake muwakilishi wa mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dkt Silas Wambura amefafanua juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mkoa wake katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Kwa niaba ya mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela mchumi wa manispaa hiyo Amosi Zephania amemuhakikishia katibu mkuu huyo wa wizara ya afya kutekeleza ushauri na maelekezo yote aliyoyaacha pamoja na kupokea pongezi alizozitoa kufuatia juhudi za manispaa yake katika uboreshaji wa huduma za afya.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.