Dozi mbili za matone ya vitamin A za kila mwaka zinaweza kuokoa maisha ya maelfu ya watoto, kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF ya mwaka 2018 imebainisha kuwa Vitamin A huimarisha mfumo wa kinga wa mtoto na kumuepusha na magonjwa hatari kama vile surua na kuhara.
Kwa kipindi cha mwezi mmoja, Halmashauri ya manispaa ya Ilemela kama ilivyo kwa halmashauri zingine imeendesha kampeni ya kitaifa ya utoaji wa matone ya Vitamini A , utoaji wa dawa kinga za minyoo ikienda sambamba na upimaji wa hali ya lishe kwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi 06 hadi miezi 59 ambapo zaidi ya watoto 77,000 wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela wamepatiwa huduma hiyo.
“Lengo katika kampeni hii ilikuwa ni kuwafikia watoto 78,406, na hadi kufikia tarehe 26 Juni tumeshatoa huduma kwa watoto 77,412 sawa na 98.7%, tunatarajia kwa muitikio huu wa wazazi hadi kufikia mwisho wa kampeni hii tutakuwa tumevuka malengo", amesema Bi Pilli Kassim, Afisa lishe wa Halmashauri ya Manispaa Ilemela alipotembelea vituo vya kutolea huduma za afya katika zahanati ya Nyakato na kituo cha afya cha Buzuruga
Aidha, Afisa lishe huyo amezitaja faida za matone ya Vitamin A kuwa ni pamoja na kuwakinga na kuwaepusha na maradhi mbali mbali yanayatokana na ukosefu wa Vitamini ‘A’ mwilini, kuimarisha uono kwa watoto na kuongeza damu.
Bi. Hawa Masinde Silima na Bi Judith mzingu wakazi wa kata ya Bizuruga ni kati ya ya wazazi waliofika kituo cha afya Buzuruga kwa ajili ya watoto wao kupatiwa huduma ya matone ya vitamini A katika nyakati tofauti wameishukuru kampeni hiyo kwani afya za watoto wao zitaimarika pamoja na kuepusha maradhi ya mara kwa mara kwa watoto wanaokosa huduma muhimu ya chanjo na matone huku wakiwahimiza wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao kupatiwa huduma ya Matone ya Vitamin A wahamasike kwani kampeni ya mwezi wa lishe inaelekea ukingoni na huduma zote zinatolewa bure katika vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma.
Bi. Juliana Martin Methew mkazi wa kata ya nyakato amesema kuwa amefurahishwa na namna wanavyohudumiwa kwa wakati na watoa huduma kwa kuzingatia weledi wa kazi, ametoa wito kwa kina baba kushirikiana na wenza wao kusimamia afya na ustawi wa watoto.
Kampeni ya utoaji wa matone ya Vitamin A chini ya kauli mbiu, "Matone ya Vitamin A ni muhimu kwa ukuaji wa maendeleo ya mtoto;tumfikie kila mtoto popote alipo" ilianza tarehe 01 juni 2025 na inatarajiwa kukamilika tarehe 30 juni 2025
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.