Na Yusuph Ludimo, Ilemela
Kamati za ujenzi wa madarasa yanayotokana na fedha za mpango wa maendeleo dhidi ya UVIKO-19 zilizotolewa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan zimetakiwa kuacha malumbano na vikwazo visivyo vya lazima ili kukamilisha kwa wakati ujenzi wa miundombinu hiyo ndani ya muda uliopangwa
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kukagua hatua za ujenzi katika shule mbalimbali zilizopo ndani ya manispaa ya Ilemela ikiwemo Kilimani sekondari, Kisundi sekondari, Bugogwa sekondari, Lumala sekondari, Shibula sekondari, Lukobe sekondari, Kabuhoro sekondari na Mwinuko sekondari ambapo akawataka wajumbe wa kamati hizo kuwa wazalendo kwa kuweka maslahi ya taifa mbele badala ya matamanio binafsi ili kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliopangwa kwa kuzingatia ubora na ufanisi unatakiwa
‘.. Tumepita baadhi ya shule unakuta wajumbe wa kamati za ujenzi wanadai posho, kwengine hakuna ushirikiano kila mmoja ana lake, Sasa hatuwezi kufika kwa namna hii, lazima tuwe wamoja tuache malumbano ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula mbali na kumshukuru Rais Mhe Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha hizo zitakazo saidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa na ile ya watoto kufata elimu katika umbali mrefu amewapongeza baadhi ya wakuu wa shule na kamati zao kwa ubunifu na matumizi sahihi ya fedha hizo kwa kujibana na kuongeza miundombinu ambayo haikuwepo katika maelekezo ya matumizi ya fedha hizo ikiwemo uongezaji wa madarasa na ofisi huku nyengine zikiwa katika hatua nzuri katika ukamilishaji wake
Kwa upande wake meya wa manispaa ya ilemela Mhe Renatus Mulunga amefafanua kuwa manispaa yake imetengewa kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia tisa na arobaini na mpaka sasa wameshapokea bilioni moja na milioni mia nane na arobaini kwaajili ya ujenzi wa madarasa huku akiahidi kusimamia matumizi ya fedha hizo na uzingatia wa ubora wa kazi itakayofanyika
Majaliwa Gerana ni Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Kilimani iliyopo kata ya Kawekamo ambae amefananua kuwa mbali na kukamilisha hatua ya upauaji wa madarasa mawili yaliyokuwa yamepangwa kujengwa katika shule yake amekumbana na changamoto mbalimbali katika ujenzi huo ikiwemo upandaji wa bei za vifaa vya ujenzi na upatikanaji wa shida wa baadhi ya vifaa ikiwemo saruji kutokana na kuhitajika na watu wengi
Manispaa ya Ilemela inatarajia kufika tamati ya ujenzi wa madarasa ifikapo Desemba 15, 2021 ambapo kila shule itatakiwa kuwa imekamilisha ujenzi huo kwaajili ya kupokea watoto wa kidato cha kwanza kwa mwaka mpya wa masomo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.