Kamati za huduma za mikopo ngazi ya kata zimetakiwa kusimamia suala zima la utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuanzia hatua ya uundaji wa vikundi sambamba na uibuaji wa miradi pamoja na kufuatilia miradi inayoenda kutekelezwa ili iweze kuleta tija katika kufanikisha dhana inayotarajiwa ya kuwainua kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Bi Ummy Wayayu ambae ni mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hizo.
“Utoaji wa mikopo hii ni utekelezaji wa sera, mikakati na mipango ya taifa katika kupunguza umaskini, kwahiyo tunapoenda kutoa mikopo hii tukalenge katika kupunguza umaskini na si vinginevyo”, amesema Bi Ummy
Kupitia mafunzo haya wajumbe wa kamati hizo wamepitishwa katika muongozo na kanuni za utengaji, utoaji na usimamizi wa mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mamlaka za serikali za mitaa ya mwaka 2024.
Akifafanua juu ya muongozo na kanuni hizo, Bi Amina Bululu ambae ni mratibu wa mikopo kwa vikundi manispaa ya Ilemela amesema kuwa, zoezi la utoaji wa mikopo kwa vikundi litafanyika kielektroniki kupitia mfumo wa maombi ya mikopo na kwamba kikundi hakitaruhusiwa kuomba mkopo mpya kama kina deni la zamani.
Aidha Bi Amina amefafanua zaidi kwa kusema kuwa kutakuwa na kamati za utoaji wa mikopo kwa ngazi za mkoa, wilaya na kata na kwamba utengaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo utafanyika kwa utaratibu wa 4;4;2 kwa maana ya kuwa asilimia nne kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu
Bi Imelda Chundu ni mtendaji wa kata ya Mecco mbali na kushukuru kwa mafunzo hayo ameomba kupatiwa nyaraka zitakazomsaidia katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za mikopo kama hadidu rejea huku Bwana Mponeja Katemi ambae ni mtendaji wa kata ya Kayenze akitaka kutengwa kwa bajeti ya uendeshaji wa shughuli za mikopo kwa ngazi ya kata
Akifunga mafunzo hayo kaimu mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii manipsaa ya Ilemela Bi Florence Vedasto amewataka watumishi wa umma kutojihusisha na mikopo hiyo na kwamba kufanya ubadhirifu wowote ni kosa kisheria hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakaebainika kuhujumu juhudi hizo za serikali katika kuwaondolea wananchi wake umasikini
Kamati ya huduma za mikopo ngazi ya kata inaundwa na mtendaji wa kata, afisa maendeleo ya jamii wa kata, afisa ustawi wa jamii, afisa elimu kata, maafisa ugani wa kata, watendaji wa mitaa ya kata husika pamoja na polisi kata.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.