Kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Mwanza imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea wilayani Ilemela.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Komredi Michael Lushinge (SMART) alipowaongoza wajumbe wa kamati katika ukaguzi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020-2025).
Wakikagua ujenzi wa kipande cha barabara chenye urefu wa Km 2.5 kitakachokamilisha Barabara ya Nyakato, Buswelu hadi mhonze inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mwenyekiti amepongeza kwa hatua iliyofikia huku akiwasisitiza TANROAD kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili kiwanufaishe wananchi wanaotumia barabara hiyo.
Kamati hiyo ilikagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kisenga iliyopo kata ya Kiseke,sambamba na ujenzi wa bweni la wasichana wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Buswelu ambapo wamempongeza Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za ujenzi wa shule hiyo ya kimkakati.
Mwenyekiti Michael (SMART) mbali na pongezi walizotoa wamemuelekeza Mkurugenzi kuhakikisha shule hiyo inakuwa na walimu wa kutosha hususan kwa masomo ya sayansi na TEHAMA. Ikiwa ni pamoja na kujenga uzio katika maeneo ya shule ili kuweza kuwalinda watoto hao na kulinda eneo la shule hizo.
Wakiwa katika kituo cha Afya cha Buzuruga kamati ilikagua jengo la mama na mtoto lilijongewa kwa mapato ya ndani ya halmashauri kamati ilipongeza na kuhimiza ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati ya Nyambiti ili iweze kupunguza wingi wa wagonjwa katika kituo hicho.
Pamoja na hayo wamewataka Wakuu wa idara na watendaji wote wa serikali kuhakikisha wanawajibika katika nafasi zao kwa kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero zao kwa wakati.
Katika nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi Ummy Wayayu wameishukuru kamati hiyo kwa ukaguzi wa miradi huku wakiahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.
Jumla ya miradi minne yenye thamani ya takriban shilingi Bilioni 3.5 imekaguliwa na kamati hiyo ya siasa ya CCM mkoa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.