Kamati ya siasa ya Wilaya ya Ilemela imeipongeza Manispaa ya Ilemela kwa utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuiagiza kukamilika miradi hiyo kwa wakati uliokusudiwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Siasa Wilaya ya Ilemela Mhe. Nelson Mesha kwa niaba ya wajumbe wote walipofanya ziara katika Manispaa ya Ilemela kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo walipata fursa ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa.
“Niwapongeze kwa juhudi ambazo mnaonyesha katika kutekeleza miradi ya maendeleo hii ni wazi kuwa mnaunga utekelezaji wa ilani ya chama, tuendelee kushirikiana ili kuweza kutekeleza ilani hii vizuri”, amesema
Katika ziara hiyo kamati imepata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Buzuruga ambayo inajengwa kwa kiwango cha ghorofa mbili kwa nguvu ya wananchi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali kuwa kila kata inatakiwa kuwa na shule ya sekondari moja.
Mwenyekiti wa kamati ya siasa pamoja na wajumbe wamepongeza jitihada za kata hiyo hasa kwa maamuzi ya kujenga ghorofa kwani itakuwa ni kata ya mfano katika Halmashauri huku wakisisitiza na kata zingine kuiga mfano huo wa ujenzi wa ghorofa huku akiahidi kuchangia mifuko kumi ya saruji ikiwa ni katika kuunga jitihada za ujenzi wa shule hiyo mpya pamoja na mifuko 10 katika shule ya sekondari ya Nyasaka ambapo pia walipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa.
Pamoja na pongezi hizo ameitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa inapima mipaka katika shule zote na kuhakikisha kuwa taasisi hizo zinakuwa na hati miliki ili kuepusha migogoro na wananchi.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe. Renatus Mulunga ambae pia ni mjumbe wa kamati hii amesema kuwa amekuwa akisisitiza sana ujenzi wa ghorofa kwani unatumia sehemu ndogo ya ardhi kuliko kutawanya madarasa ambapo hutumia eneo kubwa la ardhi na kuahidi kuwa ataendelea kusisitiza wajumbe wa baraza ambao ni madiwani kutoka kata 19 kuiga mfano wa kata ya Buzuruga.
Aidha wameweza kutembelea mradi wa usambazaji maji kutoka chanzo kipya cha Butimba ziwa Victoria wenye thamani ya Shilingi Bilioni 17 hadi kukamilika ambapo utakapokamilika unatarajia kuhudumia kuhudumia wananchi elfu 52 katika mitaa 12.
Wakiwa katika mradi huo wa maji wamepongeza jitihada za serikali pamoja na wataalam wanaosimamia mradi huo huku wakisema kuwa wanafarijika kuona kuwa mradi mkubwa kama huo unatekelezwa bila kuwa na upungufu wowote wa fedha na kushauri kuwa mradi huo ukamilike kabla au kwa wakati uliopangwa.
Nae Katibu wa chama Wilaya ya Ilemela, Aziza Isimbula ameipongeza Halmashauri kwa ushirikiano ambao imekuwa ikitoa katika kuhakikisha kuwa ilani ya Chama inatekelezwa kwa ukamilifu.
Ndugu Godfrey Mnzava, Afisa Tarafa katika wilaya ya Ilemela amekipongeza chama kwa kufikisha miaka 44 toka kilipozaliwa na kwa niaba ya serikali aliahidi kuendelea kufanya kazi kama serikali imara huku akiahidi utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa katika ziara hiyo.
Katika ziara hiyo, kamati ya siasa Wilaya ya Ilemela imekagua miradi mitano mitatu ikiwa ya serikali ambayo ni mradi wa maji, ujenzi wa shule mpya Buzuruga na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Nyasaka pamoja na miradi miwili ya sekta binafsi ambayo ni kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona pamoja kiwanda cha kuchakata mabondo ikiwa ni katika kuadhimisha miaka 44 ya Kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi ambapo kilele chake kitakuwa tarehe 06/02/2021
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.