Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela ikiongozwa na Mwenyekiti Ndugu Nelson Mesha, imeipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya Maendeleo.
Pongezi hizo wamezitoa walipofanya ziara kwa ajili ya kutembelea, kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ndugu Nelson Mesha ambae ni Mwenyekiti wa kamati hiyo alielekeza pongezi zake kwa Mkurugenzi na uongozi wa Manispaa ya Ilemela kwa utekelezaji mzuri wa miradi yenye viwango na kusema kuwa Ilemela imekuwa ikisimamia na kutekeleza vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi tangu mwaka 2015 kwani changamoto zilizokuwepo hapo awali ni tofauti na zilizopo sasa mambo mengi yameboreshwa ikiwemo utatuzi wa changamoto za migogoro ya ardhi.
Aidha akiwa katika ukaguzi wa mradi wa maji katika Tanki la maji Iramba lililopo Kata ya Nyamhongolo alisema kuwa, amesikitishwa kwa kutokukamilika kwa mradi huo na hivyo kutoa rai kwa MWAUWASA kuhakikisha kuwa mradi huo na mingine inakamilika ili uweze kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa eneo hilo la Nyamhongolo na maeneo ya jirani.
“Nitoe rai kwa MWAUWASA kuhakikisha wanakamilisha mradi huu wa maji na miradi mingine ili wananchi waondokane na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama”, alisisitiza
Nae Mbunge wa Ilemela Dkt.Angeline Mabula alisisitiza kuhusu suala la maji kwa kuwataka MWAUWASA kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi inayoendelea ili kuondoa adha ya maji kwa wananchi kwani hitaji la maji kwa wananchi wa Manispaa ya Ilemela ni Kubwa.
Nae Katibu wa kamati hiyo ya Siasa ya Wilaya, Aziza Isimbula aliipongeza Ilemela kwa kusema kuwa huwezi kuwa na miradi mizuri yenye tija kama hakuna usimamizi mzuri unaozingatia thamani ya fedha. Aliongeza kusema kuwa miradi hii waliyotembelea itakapokamilika italeta taswira nzuri kwa Manispaa ya Ilemela.
Pamoja na pongezi hizo wajumbe wa kamati hiyo walitoa maoni mbalimbali kuhusiana na miradi hiyo waliyotembelea pamoja na kutoa ushauri kwa ajili ya kuboresha hatua mbalimbali za miradi ilipofikia ili iweze kuleta tija kwa wananchi wa Ilemela.
Kamati ikiendelea na ziara hiyo ilitembelea mradi wa kimkakati wa stendi ya mabasi na eneo la maegesho ya malori eneo lililopo katika kata ya Nyamhongolo ambapo walipongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha kuweza kutekeleza mradi mkubwa kama huo ambapo ukikamilika utaleta taswira nzuri kwa Manispaa ya Ilemela pamoja na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Pamoja na hayo Mhe.Angeline Mabula ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Ilemela alisema kuwa ana imani mradi huu utakapokamilika uchumi wa Ilemela utaenda kuimarika. Aidha alitoa ushauri kwa mkandarasi wa mradi huo STECOL Corporation Ltd kuwa kazi katika mradi huo zifanyike kwa awamu yaani mchana na usiku ili kuweza kukamilisha mapema kwani lengo ni kuona mradi unaanza kufanya kazi ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Ilemela.
Aidha Ndugu Mesha amemtaka mkandarasi wa mradi kuhakikisha kuwa wanaboresha malipo ya vibarua wanaofanya katika mradi huo kwani kazi inayofanyika hapo ni kubwa ukilinganisha na malipo hayo ambayo hayaendani na kiwango cha malipo ya serikali kwa vibarua.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe Renatus Mulunga alitoa pongezi zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mbunge wa Ilemela na timu ya wataalam wa Manispaa ya Ilemela na wananchi kwa jitihada zao walizowekeza katika kuhakikisha kuwa miradi inakamilika kwa viwango vya juu.
Kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Ilemela imekagua miradi 10 inayotekelezwa na Manispaa ya Ilemela ikiwa ni utaratibu waliojiwekewa kwamba kila baada ya miezi 6 hufanya ukaguzi huo kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Miradi waliyotembelea na kukagua ni; mradi wa mzani wa mazao ya samaki, Barabara za Mwaloni, mjimwema –Bigbite, Sabasaba-kiseke-buswelu, Mradi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari Buswelu, mradi wa kimkakati wa stendi ya mabasi Nyamhongolo, Kituo cha polisi Nyamhongolo, tanki la maji Iramba na mradi wa ujenzi wa nyumba ya mwalimu shule ya msingi Nyamadoke.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.