Mwenyekiti wa kamati ya kupinga ukatili wa wanawake na watoto (MTAKUWWA) wa Manispaa ya Ilemela ndugu Leonard Masale ameitaka jamii ya Ilemela kuungana kupinga ukatili wa namna yoyote ndani ya jamii.
Akizungumza wakati wa kikao cha robo ya mwisho wa mwaka wa fedha 2023/2024 chenye lengo la kujadili utekelezaji wa mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto Masale amesema
"Ulinzi na usalama wa wanawake na watoto ni wajibu wa watu wote mahali popote walipo."
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za MTAKUWWA mratibu wa kamati hiyo Bi.Sara Nthangu ameainisha mafanikio ya kamati ni pamoja na kuundwa kwa madawati ya kijinsia 32 ya kupinga ukatili dhidi ya watoto ndani na nje ya shule, jumla ya mabaraza 24 yamejengewa uwezo wa kupinga ukatili ndani ya jamii.
Aidha jumla ya kamati 7 za ulinzi wa wanawake na watoto katika kata 7 zimejengewa uwezo sambamba na vikundi 27 vya malezi katika kata hizo 7 .
" Jamii sasa hivi imeingiliwa na vitu vingi sana vinavyomuathiri mtoto moja kwa moja kuna ubakaji,ulawiti ambao unazidi kushika kasi embu tuwalinde watoto angalau kwa kuboresha malezi na kutenga muda wa kizungumza nao kwa undani." Amesema Mzee maarufu mama Consolata Saanane.
Kamati hiyo imejadili suala la ulinzi wa watu wenye ulemavu wa ngozi huku ikitaka kuwe na mpango maalum wa kuwalinda.
" Manispaa ya Ilemela tutaendelea na mpango wa kuboresha miundo mbinu upande wa elimu maalum,mpaka sasa tutaendelea na ujenzi na ukamilishaji wa mabweni mawili kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum pamoja na watoto wenye u albino,tunaamini watoto hao watakuwa salama chini ya uangalizi maalum." Afisa elimu maalum Ilemela Bi.Sarah Ulimboka
Kamati hiyo imepinga vikali imani za kishirikina zinazohusisha vifo vya watu wenye u albino kwa mlengo wa kupata mali au vyeo vikubwa kwa viongozi wa ngazi mbalimbali.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.