Kamati ya fedha na mipango ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ndani ya manispaa hiyo lengo likiwa ni kujiridhisha na matumizi ya fedha zinazotolewa na kuelekezwa kwenye miradi ya wananchi wa Ilemela.
Akizungumza wakati wakikagua mradi wa ukarabati wa ofisi na vyoo vya mwalo wa Kayenze Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela Mhe.Renatus Mulunga amesema ni wajibu wa kamati hiyo kufanya ufatiliaji wa mara kwa mara punde fedha zinapotoka kwa ajili ya kukagua thamani ya fedha inayotumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili iweze kuleta tija kwa wananchi.
Aidha kamati imetembelea mradi wa ofisi ya serikali ya mtaa Kayenze ambayo imekaribia kukamilika ambapo ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi milioni 8 ikiwa ni fedha kutoka chanzo cha mapato ya ndani.
Wakiwa katika eneo la ujenzi wa kituo cha afya Kayenze, Mhe.Mulunga amesema “Tumepokea milioni 250 kutoka serikali kuu za hatua ya awali kuanzisha ujenzi huu,hakika tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuonyesha nia ya moja kwa moja kuanzisha na kumaliza miradi ya afya kama hii kwa manufaa ya wananchi wake,kikubwa tunataka fedha hii itumike kwa uangalifu kwa malengo yaliyokusudiwa.”
Miradi mingine iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa bweni shule ya sekondari Sangabuye ambapo kazi inaendelea vizuri ,soko la Kiloleli,Nyasaka na Kabwaro sambamba na ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa Nyambiti.
Aidha, kamati hiyo ilitoa pongezi kwa timu ya masoko ya manispaa kwa kazi kubwa wanayoendelea nayo ya kuwapanga na kuwahamishia wafanyabiashara katika maeneo rasmi ya masoko na pongezi hizo wamezitoa walipotembelea masoko yaliyoainishwa kwa ajili ya kuwapanga wafanyabiashara hao
Mstahiki meya alionyesha msisitizo kuhusu suala la kuwapanga wafanyabiashara kwa kuwahimiza waheshimiwa kuungana ili kuweza kufanikisha kwani kwa sasa suala hili ni kipaumbele kwa sasa kufuatia agizo la mMhe. Rais.
Manispaa ya Ilemela inaendelea na maboresho ya miundo mbinu ndani ya masoko yake yote kwa kasi sambamba na uwekaji wa taa ili kuweza kuruhusu biashara kufanyika hadi nyakati za usiku lakini pia ikiwa ni moja ya njia ya kuimarisha ulinzi wa mali za wafanyabiashara wake, utengenezaji wa vyoo,umwagaji wa molamu maeneo korofi na kuendelea na masuala ya ufatiliaji wa ruti za magari ya abiria kufika hadi jirani au ndani ya maeneo ya masoko yote rasmi.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.