JUKWAA LA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI LAZINDULIWA ILEMELA
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imezindua jukwaa la uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake wa wilaya hiyo ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha inawainua kiuchumi sambamba na utekelezaji wa agizo la mlezi wa wilaya hiyo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu alilolitoa mapema mwaka huu
Akimkaribisha Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa Manispaa yake kupitia baraza la madiwani itaendelea kutoa ushirikiano na kusaidia wanawake kuweza kujikwamua kiuchumi kama inavyofanya sasa kwa kutoa mapato yake ya ndani kwa kina mama na vijana waweze kujikwamua kiuchumi
Katika uzinduzi huo mgeni rasmi na mkuu wa Wilaya ya Ilemela Daktari Leonard Masale amewataka wanawake hao kulitumia jukwaa hilo katika kujadili fursa na changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi na kuwataka kutumia kama njia ya kujikwamua kiuchumi kwa kujihusha na shughuli za uzalishaji ili kuifikia Tanzania ya Viwanda.
“Kajadilini fursa na mkazifahamu changamoto kisha mshiriki katika kuzipatia ufumbuzi kwa kufanya biashara au shughuli zozote za kiuchumi, Ndugu zangu Tunalo tatizo hatupeani taarifa na hizi fursa hatuwezi kuziona kama hatupeani taarifa”, Alisisitiza
Nae Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kheri James amewahakikishia wanawake waliohudhuria uzinduzi huo kuwa Mbunge wao na naibu Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mheshimiwa Daktari Angeline Mabula pamoja na majukumu ya kitaifa aliyonayo anatambua changamoto wanazokumbana nazo na kuongeza kuwa ataendelea kuwasemea na kuwapigia katika kuhakikisha wanawake wanajikwamua kimaendeleo
Uzinduzi wa jukwaa hilo ambalo limejumuisha wanawake kutoka kata zote 19 za Manispaa ya Ilemela lilifuatiwa na uchaguzi wa viongozi wa jukwaa hilo ambapo ndugu Winfride Mgendi alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Ulowa Paulo kuwa katibu wa jukwaa hilo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.