Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia jeshi la zimamoto la Wilaya ya Ilemela imeendesha mafunzo ya siku moja kwa watumishi wake juu ya tahadhari za moto katika maeneo ya kazi na majumbani.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa hiyo kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi.Neema Semwaiko amesema ni muhimu kwa watumishi na wananchi wote kwa ujumla kufahamu tahadhari za moto ili kuweza kuepuka madhara ya moto yanayoweza kuleta hasara kubwa.
".. Mazingira yetu ya kazi tunaweza kuyaona ni mazuri ,bila ya kuwa na uelewa wa masuala ya tahadhari za moto ni hatari sana.."
Akitoa mafunzo kwa watumishi Mrakibu msaidizi Deusdedith Rutha Mkuu wa zimamoto (W) Ilemela ameainisha sababu zinazoweza kusababisha majanga ya moto ikiwemo matumizi ya vifaa vya umeme visivyo na ubora,moto wa makusudi, kutumia vifaa vingi vya umeme katika mkondo mmoja kupita uwezo wake.
Kuacha chakula kinachemka jikoni bila uangalizi pia inaweza kusababisha ajali ya moto.
"..Nawasihi wananchi wote kuchukua tahadhari kwa kuongeza umakini katika maisha yetu ya kila siku tunapotumia moto. Namba yetu ya dharura ni 114.."
Mkuu huyo wa zimamoto amewataka wananchi wote kuwa na mahusiano mazuri na kuishi kwa kusaidiana hasa katika nyakati za majanga .
Nae Coplo Jonas Burton amefafanua kuhusu mbinu za kuzima moto kwa kupoza ambapo vifaa maalum vya kuzimia moto "fire extinguisher"hutumika, kufunika moto kwa kutumia blanketi maalum au nguo iliyoloweshwa maji sambamba na kutumia mpira maalum "fire ball" unaweza kutumiwa na yeyote kwa mazingira ya moto mdogo .
Mtunza kumbukumbu katika masjala ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bi.Kubini Peter ameushukuru uongozi wa Manispaa hiyo kwa kuruhusu mafunzo hayo ambayo yamekuwa na tija kubwa kwao.
Akihitimisha mafunzo hayo Mkuu wa divisheni ya utumishi Egidy Teuras amesema mafunzo hayo ni sehemu ya kuwajali watumishi wake katika kuhakikisha kuwa wanakuwa salama na wanaelewa matumizi sahihi ya miundo mbinu mbalimbali inayowazunguka wakiwa kazini na hata majumbani.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.