Jamii imetakiwa kushiriki na kuunga mkono utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinazoendelea katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalum iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Buswelu wilayani humo litakalo gharimu kiasi cha shilingi Milioni mia moja na hamsini kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi arobaini ambapo ameiasa jamii kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kushiriki ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kuilinda, kuchangia nguvu na mali ili iweze kukamilika kwa wakati‘.. Natoa pongezi kwa wote walioibua wazo hili na wadau waliotoa michango yao ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi, Niwaombe tusimamie vizuri michango yote inayotolewa ili tuweze kukamilisha mradi huu kwa wakati ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala mbali na kumshukuru Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan kwa jitihada zake katika kuboresha sekta ya elimu amewapongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kuunga mkono jitihada hizo ambapo ametoa jumla ya tofali elfu tano na mkurugenzi wa manispaa hiyo aliyetoa tofali elfu tano mia tisa na ishirini kwaajili ya ujenzi huo huku akiwataka wadau walioahidi kuchangia gharama za ujenzi wa bweni hilo kuhakikisha wanakamilisha ahadi zao ndani ya siku saba ili kuharakisha ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Joseph Apolinary amewataka wazazi kuhakikisha wanawafichua watoto wenye ulemavu na kuwapeleka shuleni ili waweze kupata elimu itakayosaidia kuboresha maisha yao na nchi kwa ujumla huku akiahidi ushirikiano katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kupunguza kero ya muda mrefu ya ukosefu wa mabweni kwa shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum .
Sara Ng’wani ni diwani wa kata ya Buswelu amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa jitihada zake katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo huku akiahidi kuchangia kiasi cha shilingi laki mbili kama ishara ya kuunga mkono juhudi hizo.
Akihitimisha mkuu wa shule ya Buswelu Mwalimu James Wanchala amesema kuwa wadau mbalimbali wamechangia ujenzi wa bweni hilo wakiwemo chama cha walimu wilaya ya Ilemela, maafisa elimu kata, watumishi wa idara ya elimu kutoka makao makuu, walimu wakuu wa shule binafsi na zile zenye vitengo ambapo jumla ya shilingi milioni kumi na moja na laki tatu na elfu tisini na tano zimeshakusanywa kwaajili ya ujenzi wa bweni hilo.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.