Jamii imetakiwa kutumia dawa za kutibu maji au kuchemsha kabla ya kuyatumia ili kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu pamoja na magonjwa mengine ya tumbo kama kuharisha na kutapika.
Hayo yamesemwa na Bi. Rose Nyemele ambae ni mratibu wa elimu ya afya kwa umma katika Manispaa ya Ilemela wakati akizunguma na wanafunzi wa shule ya msingi Kayenze ndogo kata ya Bugogwa wakati akitoa elimu juu usafi wa mazingira,uandaaji wa chakula katika mazingira safi na matumizi ya vyoo bora.
‘.. Maji yaliyochemshwa yana harufu ya moshi na maji yaliyowekwa dawa yana harufu ya dawa, Sasa jamani hata maji yenu mnayotumia hapa shuleni yanatakiwa yatibiwe, tunaweka ndoo ya lita ishirini alafu tunaweka kidonge 1 kwa maji ya bombani,maji kutoka kwenye ziwani moja kwa moja au kwenye mito vidonge viwili. Tunatamani wote muwe salama mjijali ..’ Alisema
Zaidi ya vidonge 35,000 vya Aqua tabs vimegawiwa bure kwa taasisi za Manispaa hiyo ikiwemo shule na masoko kwa ajili ya kutibu maji wanayotumia ili kuwa kinga na magonjwa yanayotokana na kunywa maji yasiyo salama.
Kwa upande wake Afisa afya manispaa ya Ilemela Bwana Francis Deogan ametaja madhara ambayo binadamu anaweza kuyapata kwa kutotumia maji safi na salama ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu, kutapika na kuharisha huku akisisitiza kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wasiokuwa na vyoo bora na salama.
Erasto Fredrick ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kayenze ndogo ambapo ametaja hatua mbalimbali walizochukua kama shule katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika eneo lao ikiwemo kuweka utaratibu wa kutumia maji tiririka na sabuni kila mara wanapokuwa eneo la shule, kusitisha watu wanaofanya biashara ndogo ndogo za vyakula katika eneo la shule, kusafisha mazingira ya eneo la shule na kutumia vyoo safi na salama.
Manispaa ya Ilemela inaendesha operesheni za usafi, utoaji elimu na usambazaji wa dawa za kutibu maji katika maeneo yenye mikusanyiko kama kambi za wavuvi, mashuleni, masoko, minada na nyumba kwa nyumba ili kukabiliana maradhi ya tumbo na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ulioanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.