Jamii ya Ilemela imehimizwa kuzingatia lishe bora katika siku 1000 muhimu za ukuaji wa mtoto ambazo hujumisha tangu kutungwa kwa ujauzito hadi miaka miwili kwani ndio mahali msingi wa maendeleo kwa binadamu wote unapoanzia.
Akizungumza na wakazi wa kata ya Sangabuye mtaa wa Imalang'ombe wakati wa maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya mtaa (SALIM) zoezi ambalo ni endelevu Afisa lishe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Bi Pili Khasim amesema ni muhimu familia hasa kina mama kufuatilia lishe bora kwa watoto wao kwa kuhakikisha wanakula makundi yote muhimu ya vyakula kwa uwiano ulio sahihi.
".. mtoto anaekula mlo kamili ubongo wake unakuwa vizuri na hata kufundishika darasani au katika maisha ya kawaida inakuwa rahisi.."
Bi. Pili ameongeza kuwa lengo ilikuwa ni kuwafikia watoto 70 kwa kuwapatia huduma mbalimbali za afya katika mtaa huo ambapo jumla ya watoto 68 sawa na 97% ya lengo wamefikiwa na kuhudumiwa.
Elizabeth Seleman ni muuguzi katika hospitali ya Wilaya ya Ilemela iliyopo kata ya Sangabuye anasema kina mama wengi hawahudhurii kliniki kwa wakati na wengine kujifungulia majumbani hali inayopelekea baadhi ya watoto kukosa chanjo muhimu za awali punde mtoto anapozaliwa ili kujikinga na maradhi .
".. huduma hii ya mtaa kwa mtaa ni nzuri kwani inawafikia kinamama wengi wasiokuwa na utamaduni wa kwenda hospitali.."
Rahel Samwel ni mkazi wa mtaa wa Imalang'ombe yeye anapongeza uongozi wa Manispaa ya Ilemela kwa kuwasogezea huduma mbalimbali za afya na kwamba imewapunguzia safari ndefu ya kwenda zahanati ya Kabusungu.
Huduma za afya zinazotolewa SALIM ni utoaji wa elimu ya lishe,upimaji wa mzingo wa mkono kuangalia ukondefu,upimaji wa uwiano wa urefu kwa umri,uzito kwa umri,huduma za chanjo,elimu kwa wajawazito sambamba na jiko darasa.
|
|
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.