Jamii ya Ilemela imeaswa kuendelea kupinga ukatili wa aina zote unaotokea katika familia kwa kuzingatia kuwa asilimia kubwa nguzo ya familia ambayo ni mwanamke huwa ni muathirika namba moja sambamba na watoto.Jamii inatakiwa kumlinda na kumjali mwanamke kwa ustawi wa familia nzima.
Hayo yamesemwa na mgeni rasmi ndugu Isack Ngasa afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Mwanza katika kongamano la wanawake wa Ilemela kuelekea maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili duniani yanayoadhimishwa kuanzia Novemba 25,2022 hadi Disemba 10,2022 lililoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto KIVULINI-Mwanza
Akizungumza wakati wa kongamano hilo ndugu Isack amesema serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa mwanamke katika jamii ndio maana zipo jitihada za kumwezesha na kumuinua mwanamke kiuchumi ili kusimama vema kwa nafasi yake.
“Mwanamke ndie mwenye nafasi ya kuokoa taifa kwa kuzingatia kuwa ndiye anayejihusisha moja kwa moja na malezi na makuzi ya watoto,serikali imeanzisha jitihada za makusudi za kumuinua mwanamke kiuchumi kwa kutoa mikopo na kuboresha na kuanzisha shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike lengo likiwa kumuongezea nguvu na uwezo vyenye kuleta matokeo chanya kwa kuzalisha familia bora.”Amesema Isack
Nae Mkurugenzi wa shirika la KIVULINI ndugu Yassin Ally amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa makini na namna watoto wanavyojihusisha na mambo mbalimbali ya mitandao ya kijamii kwani wengi hupenda kuiga vitu bila kufikiria madhara yake baadae.
“Masuala ya mitandao ya kijamii yanaendelea kuingiza tamaduni za mataifa mengine ambazo watoto wanaiga kwa kutenda na madhara yake tunaanza kuyaona,mambo ya kulawiti,ushoga ni baadhi ya mambo watoto wetu wanaiga huko.Wazazi tuwasaidie watoto wetu kuiga mambo yenye manufaa kwao na si kila kitu .”Amesema Yassin
Aidha mwakilishi wa umoja wa wanawake wa CCM (UWT) Ilemela Bi.Herith Mdachi amesema kuwa wazazi tupunguze ubize tuwaoshe na tuwakague watoto wetu mara kwa mara,tuache kuwaita watoto majina ya ajabu na fedhea,ulawiti ishakuwa kama mtindo wa maisha tuungane kupaza sauti kupinga haya mambo kwani hata vitabu vya dini vinakataza.”
Mhe.Stella Mlacha ni hakimu mahakama ya Ilemela (kituo jumuishi) amewahusia kina mama kutambua kuwa wao ndio walezi na walinzi wa familia na wazingatie malezi mazuri kwa watoto toka wakiwa wadogo kwa kuamini kuwa mtoto hatoweza kuacha njia iliyo sahihi kirahisi.
Akihitimisha kongamano hilo Mratibu wa masuala ya kupambana na ukatili Manispaa ya Ilemela Sarah Nthangu amewashukuru wadau wote na wanawake wa Ilemela walioshiriki kongamano hilo huku akisisitiza wazazi kupunguza usiri katika masuala ya elimu ya uzazi kwa watoto na kuwafanya watoto kuwa marafiki ili wawe huru kusema chochote kinachowasibu .
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.