Na Paschalia George- Ilemela
Jamii ya Ilemela imeaswa kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu kwa kuzingatia haki ya wao kupata elimu na huduma za msingi sambamba na kuchangamana na wenzao ili kuboresha afya zao za mwili na akili.
Hayo yamesemwa na Afisa elimu wa elimu maalum Ilemela Bi. Sarah Ulimboka wakati akipokea jumla ya viti mwendo “ wheel chairs” 8 vyenye thamani ya shilingi milioni 8.1 kwa ajili ya watoto waliopo shule zinazotoa elimu maalum Ilemela kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali “ Determined Education and Rural Empowerment” DERE na Walkabout Foundation yanayofanya shughuli zake ndani ya Mkoa wa Mwanza.
“Ni jukumu letu sisi jamii nzima kuwalinda na kuwapenda watu wenye mahitaji maalum. Manispaa ya Ilemela inakaribisha wadau zaidi katika kuunga mkono juhudi za serikali kuwajali na kuwaboreshea mazingira watu hawa.Tunajua wanapitia changamoto nyingi katika kuishi kwao kutokana na ulemavu wa viungo vyao ,mimi na wewe tuwe sehemu ya kuwarahisishia maisha yao kwa namna mbalimbali tuwezavyo.” Amesema Sarah.
Nae Mkurugenzi wa shirika la DERE ndugu Jacob Odiwa amesema shirika lina furaha kuendelea kutoa huduma hizo kwa wahitaji japo hadi sasa mahitaji bado ni makubwa sana,walemavu wengi bado hawajafikiwa na huduma hizi kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wengi wao kufichwa majumbani.
“ Shirika letu la DERE linahusika na utoaji wa huduma mbalimbali wezeshi kwa watu wenye ulewamavu wa viungo.Tutaendelea kushirikiana na Halmashauri katika kuboresha mazingira mazuri ya watu hawa kwa kutoa vifaa au vitu mbalimbali kama viti mwendo vitakavyowasaidia katika maisha yao ya kila siku kadri ya uwezo wetu.” Amesema Mkurugenzi Odiwa
Ayubu Gwanchele Ngonzela (14) ni mwanafunzi katika shule ya msingi Nyamwilokelwa ,anasema anashukuru kwa kiti mwendo alichopewa ambacho kimempa matumaini mapya katika changamoto yake ya kutembea na anaamini atafanya vizuri zaidi katika masomo yake.
“ Hata sisi hatukupenda kuwa na watoto walemavu lakini Mungu ametupa,ni wajibu wetu kuwapenda na kuwajali .Nawasihi wazazi wenzangu wenye watoto wenye changamoto kama hizi msiwafiche maana mnawakosesha fursa nyingi.Wapo walemavu ambao wanafanya vitu vikubwa vya kustaajabisha jamii.Nawashukuru sana kwa mwanangu kupata baiskeli kwani itamrahisishia mizunguko yake ya hapa na pale.Mungu awabariki sana” Amesema Sophia Charles mzazi wa Ayubu.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.