Malezi na makuzi ya watoto ni jukumu la jamii nzima kuanzia ngazi ya familia ikihusisha wahusika wakuu baba na mama katika kuhakikisha familia inakuwa salama na kuondoa mazoea ya kumwachia mama kila kitu hali inamfanya kuwa na majukumu mengi wakati mwingine kumzidia.
Hayo yamesemwa na Katibu tawala Msaidizi,Mipango na uratibu Mkoa waMwanza ndugu Shilungi Ndaki wakati wa kikao cha mrejesho na kuthibitisha matokeo ya utafiti juu ya Mwingiliano kati ya malezi na ustawi wa mtoto na uwezo wa mwanamke kufanya chaguo na maamuzi yanayotambuliwa na kuheshimiwa,utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali Tanzania Home economics Organization (TAHEA –Mwanza) ndani ya Halmashuri ya Manispaa ya Ilemela ikihusisha kata mbili za Bugogwa na Sangabuye.
“ ..Nawapongeza sana TAHEA na washiriki wote waliofanikisha utafiti huu,najua sio kazi rahisi na najua mwisho wa tafiti ni mwanzo wa tafiti nyingine kubwa ni kwa wataalam kuhakikisha tunaelewa ili iwe rahisi kufikisha ujumbe kwa jamii zetu tunazozihudumia..”
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utafiti huo Mtafiti Lorraine Kiswaga amesema utafiti umeonyesha malezi ya watoto ni muhimu sana ndani ya siku 1000 za mwanzo tangu kuzaliwa kwa mtoto kwani ni wakati ambao akili ya mtoto inakuwa hivyo ni lazima kutengeneza mazingira mazuri yatakayochochea makuzi na malezi imara.
Aidha Bi.Lorraine amesema lengo la utafiti huo ni kuelewa zaidi kuhusu vipengele mbalimbali vinavyoathiri maisha na fursa za wanawake,kuangalia uwezo wa mwanamke kushiriki katika masuala ya kiuchumi yanayoweza kuathiri utolewaji wa huduma za kijamii kama lishe bora kwa mtoto huku akibainisha changamoto ya kina mama kushindwa kutoa majibu kwa maswali ambayo majibu yake wanayafanyia kazi na kuyaishi kila siku katika maisha yao ya kawaida kama vile kunyonyesha watoto wao.
“..serikali izidi kuboresha sera na miongozo katika kuwawezesha wanawake kiuchumi ,kupata ulinzi wa kisheria na kuongeza huduma ya afya ya akili itakayoweza kusaidia jamii hasa wanawake wanaopitia changamoto mbalimbali katika malezi ya watoto..” Amesema Bi.Lorreine
Janeth Paulo ni mzazi kutoka mtaa wa Igumamoyo uliopo kata ya Sangabuye yeye anapongeza wadau na wataalam kufika kwenye maeneo yao huku akitoa rai ya tafiti zinazofanyika zitoe uelewa na muelekeo wa namna ya kuishi kwani watu wengi hawajui cha kufanya.
“..Mi nilijua ni sawa tu kwa mwanamke kuwa na majukumu yote kwa sababu ndivyo tulivyozoea,mwanaume yeye afanye anavyotaka kwa sababu amekuoa ndo tunajikuta tunaingia kwenye vishughuli shughuli,vicoba ili watoto wale waende shule na wao wajipambanie ndoto zao ..”
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.