Jamii imetakiwa kuepukana na uharibifu wa mazingira na kuweza kuruhusu urejeshwaji wa ardhi ambayo imeshaharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa kupanda miti, kuhifadhi bionawari kwa kuepuka kuchoma misitu au mashamba katika uandaaji wa mashamba au mavuno.
"Takribani asilimia 40 ya ardhi yote duniani imeshaharibiwa uharibifu unaokadiriwa kuathiri zaidi ya watu Bilioni 3 ifikapo mwaka 2050 hivyo ni lazima tubadilike ."
Kauli hiyo imetolewa na mhadhiri wa chuo kikuu cha SAUT Mwanza Dr.Emmanuel Lwankomezi wakati wa kongamano la kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani alipokuwa akiwasilisha mada ya Urejeshwaji wa Ardhi.
Ameongeza kusema kuwa ili kuweza kurejesha ardhi iliyokwisha haribiwa jamii inapaswa kupanda miti, kuhifadhi bioanuwai kwa kuepuka kuchoma misitu au mashamba kipindi cha uandaaji wa mashamba au mavuno.
Akiwasilisha mada ya nishati safi teknolojia rafiki kwa mazingira Mkurugenzi wa Chabri energy Co.Ltd Bernard Makachia amesema ni wakati wa jamii kuangalia nishati mbadala za kutumia majumbani ili kuepuka uharibifu na uchafuzi wa mazingira.
"Jamii nzima tunalo jukumu la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,tumieni nishati inayotokana na taka ngumu hapo tutaweza kutunza taka zetu vizuri kwa kutambua thamani yake na wakati huo huo tutapata nishati yenye nguvu na salama kwa mazingira yetu." Amesema Makachia
Akichangia katika kongamano hilo Asha Stephen ambae ni mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Lukobe amewashukuru waandaji wa kongamano hilo kwani amejifunza namna bora ya kuepuka mmonyoko wa udongo kwa kupanda miti.
Mratibu wa Roots & shoots kanda ya ziwa Bi.Leticia Mlawa ameunga hoja juu ya utunzaji wa mazingirana kusema kuwa kuwa ipo haja ya kupanda miti ili kuweza kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwani ni rahisi kutunza miti kuliko kupanda miti .
Nae Afisa mazingira kutoka Ilemela Ndugu Phinias Marcon amebainisha kuwa Jumla ya miti 40,727 imepandwa maeneo ya umma na binafsi ikiwemo miti ya matunda,vivuli na mbao katika kuhakisha mazingira yanahifadhiwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 05 juni, Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imeendesha kongamano lililowajumuisha wadau mbalimbali wa mazingira wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, shule za sekondari na msingi chini ya kauli mbiu “Urejeshwaji wa Ardhi,ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame”.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.