Manispaa ya Ilemela imezindua awamu ya pili ya upimaji wa Saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake bila gharama yoyote zoezi litakaloendeshwa katika vituo vya afya vya Sangabuye na Buzuruga kuanzia Julai 01 hadi Julai 05, 2019.
Akizindua zoezi hilo la upimaji, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mheshimiwa Daktari Angeline Mabula ameishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kutoka chuo kikuu cha Calfornia nchini Marekani kwa kuendesha zoezi hilo litakalosaidia kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Saratani sanjari na kurithisha ujuzi kwa wataalam wazawa watakaoendelea na utoaji wa huduma mara baada ya kuisha kwa kampeni ya pamoja.
‘.. Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Magufuli kwa uboreshaji wa sekta ya afya, Kwa wilaya yetu upatikanaji wa dawa ni zaidi ya asilimia 95 niwatoe hofu mkishagundulika kuugua ugunjwa huu tiba ipo, Kikubwa niwaombe mkawe mabalozi wazuri kwa wengine mhamasisheni waje kupima wapate tiba ..’ Alisema
Aidha Mheshimiwa Mabula amevitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinahamasisha jamii kujitokeza kupata huduma hiyo sambamba na kuwatoa hofu wananchi kutokata tamaa pindi watakapogundulika kuugua ugonjwa wa Saratani kwani Serikali imejidhatiti kupambana nao kwa kuhakikisha wataalamu na madawa vinapatikana kwa urahisi.
Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Ilemela Daktari Florian Tinuga amesema kuwa zoezi la upimaji wa Saratani ya mlango wa kizazi kwa awamu ya pili litaendeshwa kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Kitengo cha Saratani cha Hospitali ya Rufaa ya Bugando na Hospitali ya Ocean Road ili kuongeza ufanisi na kupunguza usumbufu kwa wagonjwa watakaobainika kuhitaji kuendelea na matibabu zaidi tofauti na ilivyofanyika kwa mara ya kwanza.
Katika nchi ya Tanzania inakadiriwa kuwa kuna wagonjwa wapya wapatao 50,000 wa Saratani ya mlango wa kizazi kila mwaka huku takwimu za wilaya zikiainisha kati ya mwaka 2018 wanawake 2047 waliochunguzwa , 384 sawa na asilimia 8.5% waligunduliwa kuwa na dalili za awali za Saratani ya mlango wa kizazi, huku chanjo ya ugonjwa huo kwa wasichana ikitolewa bure kwa wenye umri kati ya miaka 9 mpaka 14.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela
Postal Address: 735 MWANZA
Telephone: + 255 736 200910
Mobile:
Email: md@ilemelamc.go.tz
Copyright ©2017 Ilemela Municipal Council . All rights reserved.